Monday, August 08, 2016

WAZIRI MKUU AIAGIZA WIZARA YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KUWACHUKULIA HATUA WATENDAJI WOTE WALIOHUJUMU USHIRIKA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananachi wakati lipotembelea maonyesho ya wakulima Nanenane kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya Agosti 8, 2016. Kushoto kwake ni mkewe Mary

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inafufua sekta ya ushirika na kuwachukulia hatua kali watendaji wote waliohujumu ushirika na kusababisha machungu kwa wanaushirika ili iwe fundisho kwa wengine.

Pia ameitaka Wizara hiyo kupitia upya sekta ya ushirika kwa kuanza na viongozi walipo ndani ya wizara hadi mikoani kuhakikisha kama wanafanya kazi zao ipasavyo na kuwaondoa watakaobainika kwa uzembe.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo leo (Jumatatu, Agosti 08, 2016) wakati akifunga maadhimisho ya sherehe za nane nane kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika kwenye uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema mkulima, mfugaji na mvuvi mdogo au mmoja mmoja hawezi kupunguza umaskini bila ya kuwa na chombo cha kuwaunganisha na kuwapa nguvu ya kutetea bei ya mazao yao kama ushirika. Aidha, ushirika imara utawasaidia kutafuta soko, kupata mikopo ya riba nafuu.

Amesema pamoja na umuhimu wa kuwepo kwa ushirika, tasnia hiyo imewaumiza wakulima wengi na kuwafanya kukata tamaa katika uzalishaji kutokana na usimamizi mbovu, ubadhirifu na ubabe wa baadhi ya viongozi wa ushirika.

“Wahimizeni na kuwashawishi wakulima, wafugaji na wavuvi kujiunga katika vikundi vya ushirika vya uzalishaji na SACCOS. Aidha, elimu ya ushirika inayotolewa kwenye maonesho ya mwaka huu, iwe changamoto kwenu kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu,” amesema.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali haitamvumilia mfugaji anayelisha katika maeneo ya hifadhi na vyanzo vya maji, Wakuu wa Mikoa na Wilaya waendelee kulinda maeneo hayo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha alisema sekta ya kilimo imekuwa na mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka mine mfululizo nchi imeweza kuzalisha chakula cha ziada, ambapo kwa mwaka huu imezalisha kwa asilimia 123.

“Mafanikio hayo yanachangiwa jitihada za Serikali katika kutoa ruzuku ya pembejeo, taasisi za utafiti ambazo zimekuwa zikitafiti aina bora ya mbegu zikitafuta mbegu bora na wakulima walioamua kuwekeza kwenye kilimo,” alisema.

Naibu Waziri Ole Nasha alisema katika ukanda wa Nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ni nchi mbili tu za Tanzania na Zambia kati ya nchi 15 za jumuia hiyo hazikabiliwiu na baa la njaa.

Licha ya mafanikio hayo Naibu Waziri huyo aliwaomba wakulima kuendelea kuzalisha kwa kufuata kanuni bora za kilimo pamoja na kutumia pembejeo bora.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ladislaus Mwanakatwe ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuwatetea pamoja na utatuzi wa kero za muda mrefu zilizokuwa zinawakabili wakulima ikiwemo ya tozo.

Hata hivyo Mwanakatwe ameiomba serikali kuitafutia ufumbuzi changamoto ya upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo. Pia ameomba Serikali iwezeshe Benki ya Kilimo (TADB) kufungua matawi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ili wakulima wake waweze kupata mikopo kwa urahisi.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMATATU, AGOSTI 08, 2016.
Post a Comment