Thursday, May 08, 2014

SERIKALI KUFUNGA MFUMO WA KIELEKTRONIKI KUJAZA MAFUTA MAGARI NA MITAMBO YA TAASISI ZA UMMA

1 (1)Mkurugenzi wa Ununuzi na Ushauri toka wakala wa huduma ya Ununuzi  Serikalini (GPSA) Bw. Yoswam Nyongera akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu uwezo wa mfumo wa kielektroniki utakaotumika kujaza mafuta katika magari na mitambo ya Serikali ikiwemo kutunza kumbukumbu za malipo ya mafuta na hivyo kutoa mafuta kwa kadiri ya fedha iliyolipwa na Taasisi husika.
2 (1)Mkurugenzi wa Uendeshaji  toka wakala wa huduma ya Ununuzi  Serikalini (GPSA) bw. Naftal Singwejo akieleza kwa waandishi wa habari  kuhusu mfumo mpya wa kielektroniki utakaotumika katika  kutoa huduma ya mafuta kwa magari ya Serikali na mitambo ili kuongeza tija  katika utoaji wa huduma hiyo kwa Taasisi ,Wakala na Wizara zote .kushoto ni Mkurugenzi Himili Biashara Bw. Malik Aram.
(Picha zote na MAELEZO)
Frank Mvungi-Maelezo
Serikali yaanza kutekeleza mradi wa kufunga mfumo wa kielektroniki kujaza mafuta magari na mitambo ya taasisi za Umma ili kuongeza tija katika  utoaji huduma hiyo kote nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) bw. Naftal Singwejo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua Singwejo amesema mradi huo utashirikisha Wizara,Taasisi zote za Umma,Wakala na Idara zinazojitegemea ambazo kwa mujibu wa sheria ya ununuzi wa Umma na 7 ya Mwaka 2011 sura ya 410 kifungu cha 56 zinatumia huduma hiyo toka kwa wakala huo.
“Hatua za awali za utekelezaji wa mradi huu zitahusisha kufungwa kifaa maalum (identification tag) katika mlango wa tanki la gari au mtambo “alisema Singwejo
 Akizungumzia faida za mfumo huo, Singwejo alisema hakutakuwa na mfanyakazi (Pump Attendant) wa kuweka mafuta katika gari au mtambo na hivyo huduma hiyo itapatikana kwa haraka na hivyo kuongeza tija.
 Faida nyingine ni kuwa taarifa ya matumizi ya mafuta ya chombo cha umma itapatikana kwa wakati kwa njia ya mtandao na hivyo maamuzi sahihi kufanyika juu ya matumizi ya mafuta kwa chombo husika.
Aidha, Singwejo alibainisha kuwa mfumo huo utaondoa kabisa udanganyifu wa matumizi  ya mafuta katika magari na mitambo kwa taasisi za umma na kutoa nafasi kwa chombo kilichodhibitika tu kuweza kupata huduma ya mafuta.
Naye Mkurugenzi Himili Biashara Bw. Malik Aram alisema kuwa mfumo huo ni wa kisasa ambao unatumika katika nchi zilizoendelea na majaribio ya mfumo huo hapa Tanzania yatafanyika katika kituo cha Kurasini mwishoni mwa mwezi Julai, 2014 ambapo hadi sasa mfumo huo umeanza kusimikwa katika kituo hicho.
Bw. Malik aliongeza kuwa baada ya kukamilika kwa mfumo huu katika kituo cha Mafuta cha kurasini katika mwaka huu wa fedha katika mwaka ujao wa fedha mfumo huo utafungwa katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa, Mbeya, na Mwanza.
Serikali ilianzisha wakala wa Huduma ya ununuzi Serikalini (GPSA) ili kudhibiti matumizi ya fedha za umma yanayofanyika kupitia ununuzi wa vifaa mbalimbali na mafuta kwa ajili ya magari na mitambo  ya umma, hivyo mfumo huu ni moja ya hatua za utekelezaji wa mpango huo kamambe wa kuwa na matumizi ya rasilimali za umma wenye tija.

No comments: