Monday, August 21, 2017

WABUNGE WA MAREKANI WAIPONGEZA TAYOA


 Kaimu Balozi wa Marekani Dk. Inmi Patterson akisailimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Vijana Tayoa, Balozi Charles Sanga alipowasili kwenye viwanja vya shirika hilo Bahari Beach Dar es Salaam pamoja na ujumbe wa wabunge watano wa Bunge la Congress la Marekani.
Ujumbe wa wabunge watano wa Bunge la Congress la Marekani wakiangalia ngoma za asili mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za Shirika la Vijana Tayoa Bahari Beach Dar es Salaam.
 Kaimu Balozi wa Marekani,  Dk. Inmi Patterson, wa kwanza kushoto akifurahia jambo na ujumbe wa wabunge watano wa Bunge la Congress la Marekani wakati wanazindua redio ya kuelimisha vijana kuhusu mbalimbali kwenye Shirika la Vijana Nchini Tayoa. Wapili kulia ni Mkurugenzi wa Tayoa Peter Masika.
 Vijana wa kikundi cha ngoma za asili wakiburudisha ujumbe wa wabunge watano wa Bunge la Congress la Marekani waliotembelea Shirika la Vijana nchini Tayoa Bahari Beach Jijini Dar es Salaam.
 
Na Mwandishi Wetu
UBALOZI wa Marekani nchini, umesifu kazi zinazofanywa na Shirika la Vijana Nchini (Tayoa), katika kuwainua na kuwahamasiha vijana kujikwamua kiuchumi na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.

Hayo yalisemwa jana na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk. Inmi Patterson, wakati ujumbe wa wabunge watano wa Bunge la Congress la Marekani wakiwa na familia zao, ulipotembelea ofisi za Shirika hilo zilizoko Bahari Beach, jijini Dar es Salaam.

Wabunge hao wa Congress walioambatana na Kaimu Balozi wa nchi hiyo ni pamoja na Carly Paul, Bob Goodlatte, Steve King, Blake Farenthold, Mike Bishop na Sheila Jackson Lee.

 Wabunge hao walijionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Shirika hilo ikiwemo elimu ya bure kuhusu masuala ya Ukimwi kupitia simu za bure, ujasiriamali na miradi mbalimbali ya kuinua vijana.

Balozi alisema yeye na ujumbe wake wamefurahi kuona kazi kubwa zinazofanywa na Tayoa kwa kushirikiana na taasisi za Marekani kama Kituo cha Kudhibiti Maradhi cha Center for Disease Control (CDC).

“Tumefurahi sana kuona kazi zenu na hasa mnavyowashirikisha vijana katika kujikwamua kiuchumi na kutafuta maendeleo, nawapongeza sana Tayoa kwa kazi kubwa mnayofanya,” alisema

Alisema Tanzania na Marekani zimekuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa muda mrefu ambao umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka na kuahidi kuwa serikali hizo mbili zitaendelea kushirikiana.

“Inafurahisha sana kuona vijana ambao wanaelimika kupitia vijana wenzao kama wanavyofanya Tayoa, vijana ambao wako tayari kushirikiana na wenzao kuleta maendeleo yao wenyewe na maendeleo ya taifa lao,” alisema

 Mmoja wa wabunge hao, Sheila Jackson Lee, alisifu ubunifu ulioonyeshwa na shirika hilo katika kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo wa kutoa elimu bure kuhusu ugonjwa wa Ukimwi kupitia simu za bure.

“Mkurugenzi wa Tayoa Peter Masika na Mwenyekiti wa Bodi ya Tayoa Balozi Charles Sanga mmefanyakazi kubwa sana, mmetumia muda wenu mwingi kusaidia maendeleo ya vijana, hii kazi mnayofanya si kwa manufaa ya watanzania tu bali dunia nzima,” alisema mbunge huyo

Alisema Tayoa imekuwa mstari wa mbele kuondoa unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi hali ambayo imesaidia wengi wao kuishi maisha ya matumaini na kujiona wako sawa na wasio na VVU kwenye jamii wanayoishi.

“Marekani ni rafiki wa Tanzania na itaendelea kuwa rafiki kwa kufanyakazi pamoja kama tunavyofanya sasa kupitia shirika letu la CDC ambalo linasaidia miradi ya afya hapa Tanzania nawapongeza sana Tayoa kwa kazi kubwa mnayofanya kuelimisha kuhusu Ukimwi,” alisema

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tayoa, Peter Masika, alisema wabunge hao wamekuja kuangalia kazi zinazofanywa na Shirika hilo na namna wanavyotumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kuelimisha vijana masuala mbalimbali ikiwemo Ukimwi kwa njia ya simu bila malipo.

“Wamefurahia sana kazi tunazofanya kwa mfano kwenye huduma za elimu ya Ukimwi kwa njia ya simu simu ambapo kila siku tunahudumia watu 2,000 na mpaka sasa tumehudumia watanzania milioni tano ambao wamepata taarifa sahihi,” alisema Masika.

No comments: