Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akimkabidhi leseni ya usajili wa Gazeti la Daily News mwakilishi wa gazeti hilo Bi. Pudenciana Temba. Idara ya Habari imetoa imetoa leseni nne kwa ambapo leseni namba moja imetolewa kwa Jarida la Nchi Yetu linalotolewa na Idara hiyo, namba mbili imetolewa kwa HabariLeo, namba tatu Dailynews na nne imetolewa kwa Spotileo.Katikati ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Usajili Bw. Patrick Kipangula.
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akimkabidhi leseni ya usajili wa Gazeti la HabariLeo mwakilishi wa gazeti hilo mhariri wa gazeti hilo Bw. Amir Mhando leo Jijini Dar es Salaam. Leseni hiyo imetolewa kufuatia kuanza kwa matumizi ya sheria mpya ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayomiliki magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo Dkt. Jim Yonaz akisisitiza jambo mara baada ya kumalizika kwa zoezi la kutolewa kwa Leseni za magazeti ya Kampuni yake kumalizika leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akimpongeza Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayomiliki magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo, Dkt. Jim Yonaz kwa Kampuni yake kuzingatia matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kwa kujisajili upya na kupatiwa leseni.
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiwa katika picha ya pamoja na wahariri wa magazeti ya HabariLeo, DailyNews, SpotiLeo yanayomilikiwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) pamoja na uongozi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mara baada ya kukabidhiwa Lesini za usajili wa magzeti hayo leo Jijini Dar es Salaam.
Picha zote na: Frank Shija – MAELEZO
…………………….
Na. Neema Mathias na Paschal Dotto- MAELEZO.
Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO) imeanza rasmi utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari kwa kutoa leseni kwa vyombo vya machapisho yakiwemo Magazeti na Majarida.
Akizungumza katika makabidhiano ya leseni hizo Jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amesema utoaji wa leseni ni utekelezaji wa agizo rasmi lililotolewa Agosti 23, 2017 lililowataka wamiliki wote wa machapisho kujisajili upya na kupewa leseni kwa lengo la kuifanya tasnia ya Habari kuwa taaluma rasmi kama zingine.
“Leseni hizo zimeanza kutolewa rasmi Agosti 23 na zoezi hilo litaendelea hadi Oktoba 15, 2017 na baada ya hapo wale amabo watachapisha magazeti na majarida bila kuzingatia Sheria hiyo watakuwa wametenda kosa la jinai”, alisema Dkt. Abasi.
Katika zoezi hilo Dkt. Abbasi alitoa leseni kwa vyombo vinne ambavyo ni Jarida la Nchi Yetu linalomilikiwa na Idara ya Habari MAELEZO, gazeti la Daily News, Habari Leo pamoja na Spoti Leo ambayo ni magazeti ya Serikali.
Dkt. Abbasi ametoa wito kwa vyombo vingine vya habari ambavyo bado havijaanza taratibu za upataji wa leseni visisubiri hadi dakika za mwisho za mchakato huo ili kuepuka msongamano na usumbufu usio wa lazima.
“Nitumie fursa hii kuwaalika ambao hawajapata leseni wafanye haraka, Tanzania Standard Newspaper (TSN) walitimiza masharti ndani ya siku tatu ndio maana leo wamepata leseni hizo, hakuna urasimu wala nia mbaya ya kufungia baadhi ya machapisho kama wengi wanavyodai bali ni katika kutekeleza matakwa ya Sheria”, alisisitiza Dkt. Abbasi.
Kwa upande wake Mhariri Mtendaji wa TSN Dkt. Jim Yonazi ameviasa Vyombo vingine vya Habari kutekeleza agizo hilo ili kupata uhuru mpana katika uwajibikaji pamoja na kuwa mfano wa kutii Sheria bila shuruti ili taaluma ya habari iendelee kuheshimika kwa jamii.
“Ukifanya kazi kihalali unakuwa na uhuru wa kufanya kazi vizuri, ubunifu unaongezeka na unafanya biashara bila wasiwasi”, alisisitiza Dkt.Yonazi.
Comments