Serikali ya Marekani yarejea upya ahadi yake ya kufanya kazi na jeshi la wananchi wa Tanzania katika mapambano dhidi VVU/Ukimwi

1
2
3MR
Dar es Salaam, TANZANIA.  Serikali ya Marekani kupitia Taasisi ya kijeshi ya Walter Reed (WRAIR) imesaini upya makubaliano ya ushirikiano na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) siku ya Jumanne, Agosti 29, 2017 katika sherehe ya kusaini tamko la pamoja la ushirikiano katika jitihada za kupambana na VVU/UKIMWI. WRAIR ni kitengo cha kikosi cha jeshi la Marekani kinachojihusisha na tafiti za kitabibu na kimefanya kazi moja kwa moja na JWTZ tangu mwaka 2004 kutekeleza programu za VVU/UKIMWI Tanzania.

Utiaji saini huo uliofanywa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dr. Inmi Patterson na Mkuu wa Huduma za Kitabibu wa JWTZ, Meja  Generali (Dk.) Denis Raphael Janga, unawakilisha dhamira ya pamoja katika upatikanaji endelevu wa huduma za afya na mpango mkakati wa kukabiliana na tishio la VVU/UKIMWI.

Makubalino ya awali, yaliyosainiwa mwaka Aprili 2011 yanabainisha ushirikiano wa pande hizo mbili katika kupunguza maambukizi mapya na kuboresha matibabu na huduma za kuzuia maambukizi.

Kupitia ushirikiano huu endelevu wa pande hizi mbili Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) unatoa nafasi kwa majeshi ikiwemo JWTZ kuelewa vizuri tishio la afya, tabia na mazingira hatarishi yanayohusiana na kuenea kwa maambukizi ya VVU.

“Mafanikio ya ushirikiano wa WRAIR/JWTZ hayapingiki na faida zake ziko wazi.”alisema Kaimu Balozi Patterson. “Kwa pamoja tumehakikisha upatikanaji endelevu wa huduma za tiba kupitia ujenzi wa vituo vipya, ukarabati wa vituo vya zamani, vya matunzo na tiba na kutoa vifaa vya maabara.”

Ushirikiano huu wa pande mbili kati ya WRAIR na JWTZ umeundwa kuimarisha na kusaidia utafiti na utekelezaji wa jitihada za matunzo na matibabu ya VVU nchini Tanzania.

Comments