RC TABORA KUWAKABA KOO VIONGOZI WA SACCOS WANAOKULA FEDHA ZA WANACHAMA


Na Tiganya Vincent-RS –TABORA

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeiagiza Maafiza kuhakikisha wafanya ukaguzi katika Vyama vya Ushirika Vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) ili kuridhisha kama fedha walizoweka wanachama zipo au hazipo iweze kuwachukulia hatua kali.

Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri katika nyakati tofauti alipokuwa akiongea na wajumbe Jukwaa la Ushirika na wakati wa Sherehe ya kuwaaga walimu walistaafu kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma.

Alisema kuwa amelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa watumishi wakiwemo walimu kuwa wamekuwa wakiweka fedha katika SACCOS kama sehemu ya kujiwekea akiba lakini wanapohitaji kukopa wanaambiwa fedha hazipo.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora alisisitiza Mtu atakayebainika kula fedha za wanachama wa SACCOS hajiandae kufikishwa katika vyombo vya Sheria ili kujibu masharti.

“Niwaagiza Maafisa Ushirika waende wakakague SACCOS zote…haiwezekani Serikali ifikishwe hapo na ibaki kimya”alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.

“Ukaguzi huo ni pamoja na kuangalia Viongozi waliopo katika SACCOS wamekopa kiasi gani na wanalipa kwa mfumo gani isije ikiwa wanaonufaika ni viongozi tu” aliongeza Mwanri.

Aliongeza kuwa baada ya ukaguzi huo Ofisi yake itayafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua mbalimbali wale wote watakaonekana kutumia vibaya madaraka yao katika SACCOS.

Naye Kaimu Afisa Ushirika wa Wilaya ya Urambo Hilda Boniface akisoma risala ya wanaushirika alisema kuwa baadhi ya SACCOS zimekufa kwa sababu ya viongozi wake ikiwemo Wakurugenzi Watendaji kushindwa kupeleka makato ya fedha za wanaushirika katika sehemu husika.

Alisema kuwa hali hiyo imewakatisha baadhi ya wanaushirika na kuwafanya wasione umuhimu wa kujiunga na SACCOS katika maeneo yao.

Comments