Vitu ambavyo hauruhusiwi kusafiri navyo kwenye ndege


Na Jumia Travel Tanzania

Kama umeshawahi kusafiri kwa ndege naamini utakuwa unafahamu ni kitu gani cha kubeba kwenye begi lako na kipi sio. Endapo haujawahi au unatarajia kufanya hivyo kwa siku za hivi karibuni basi usafiri huo una masharti na taratibu zake ambazo ni lazima zifuatwe vinginevyo hautoweza kuutumia.

Tofauti na usafiri wa kawaida kama vile mabasi ambayo watanzania wengi tunayatumia ambapo ni mara chache kukuta kunakuwa na upekuzi mkali wa abiria mbali na tiketi zao, Jumia Travel ingependa kukufahamisha kwamba kusafiri kwa kutumia ndege kuna masharti na taratibu ambazo kila abiria ni lazima azifuate na kuzizingatia ndipo aruhusiwe kuingia ndani.  

Vifaa vyenye ncha kali.Hairuhusiwi kabisa kubeba vitu vyenye ncha kali kama vile kisu, wembe, mkasi, bisibisi au panga kwenye begi lako la kusafiria labda iwe kwenye mzigo tofauti ambao utapekuliwa na kupewa kibali. Kwa ufupi kama unadhani utahitajika kuvibeba ni vema kuviweka kwenye mzigo tofauti ili vifanyiwe upekuzi ndipo uruhusiwe. Tofauti na hapo ili kuepuka usumbufu au kuchelewa safari yako basi unashauriwa kuwasiliana mapema na shirika la ndege utakalosafiri nalo kwa msaada zaidi.      

Silaha za moto. Hakuna silaha inayoruhusiwa kubebwa kwenye begi lako la kusafiria kwa sababu za usalama wako na abiria wengine kwenye ndege. Ingawa taratibu hutofautiana baina ya nchi au mashirika ya ndege lakini asilimia kubwa vitu hivyo huwa haviruhisiwi kabisa labda kuwa na sababu na kibali maalumu.   

Vitu vinavyoweza kulipuka.Kuna baadhi ya bidhaa tunazitumia ambazo ndani yake zina kemikali ambazo hulipuka kwa urahisi bila ya kujua. Kwa mfano, takribani marashi yote ya kujipulizia mwilini (body spray) au vibiriti vya gesi huwa na kemikali ambazo zinaweza kulipuka kwa urahisi na ndiyo maana huwekwa alama ya moto (inflamable). Hivyo basi ni vema kulijua hilo ili unaposafiri usibebe maana utaishia kwenda kuyaacha mahala pa ukaguzi kabla ya kupanda ndege.

Vifaa vya michezo. Kuna baadhi ya vifaa vya michezo vinachukuliwa kama silaha. Kwa mfano, vifaa vya kuchezea gofu, tenesi, mpira wa magongo, upinde na mkuki na kadhalika. Kwa mfano, timu nyingi za michezo mbalimbali zinaposafiri vifaa hivi huwekwa kwenye mizigo tofauti na ile ya wachezaji kwa ajili ya ukaguzi ili kuepusha usumbufu.

Vifaa vya kazi. Inawezekana ukawa ni fundi mzuri na una wateja takribani kila kona ya nchi hivyo ukahitajika kusafiri kwenda kufanya kazi. Itakuwa ni jambo la busara ukafahamu mapema kwamba kusafiri kwenye begi lako na vifaa vyako vya kazi kama vile nyundo, msumeno, patasi au bisibisi itakuwa ngumu. Utaweza kufanya hivyo pale tu utakapovifungasha kwenye mzigo wake tofauti ili ukaguliwe kwa ajili ya usalama wako.   

Dawa za binadamu. Kuna wakati unaweza ukawa na matatizo ya kiafya lakini ukahitajika kusafiri hivyo ni vema kujua pia kuna taratibu za kusafiri na dawa zako za matibabu. Iwe unasafiri ndani au nje ya nchi vitu muhimu vya kuzingatia ni pamoja na barua au maelezo ya daktari kuhusu ugonjwa wako pamoja na dawa alizopendekeza kuzitumia na kubeba. Kwa hiyo ili kuepuka kuzuiwa kusafiri na dawa wakati mwingine itakuwa vizuri hata ukawasiliana na shirika la ndege utalosafiri nalo ili ujue taratibu zao zikoje.

Vimiminika. Unaweza ukashangaa kwanini hautoruhusiwa kusafiri na maji yako ya kunywa ambayo umeyabeba kwenye begi lako. Ingawa sheria hutofautiana kwa baadhi ya nchi ambazo huruhusu kiwango fulani kwa hapa Tanzania hali ni tofauti. kwenye kundi hili maziwa ya chupa na madawa hayaingii kwenye kundi hili ingawa ni lazima yaambatinishwe na maelezo au kibali maalum.     

Bangi. Nadhani hili linaeleweka miongoni mwa watu wengi kwamba Tanzania kilevi hicho ni marufuku kukitumia kwa hiyo kukutwa nacho tu ni uvunjaji wa sheria. Kuna baadhi ya nchi zinaruhusu aina ya kilevi hicho kana kwamba mpaka madaktari hutoa vibali kabisa kwa wagonjwa wao kutumia. Ila kwa nchi ya Tanzania bangi ni marufuku na ukikutwa nayo utachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa kawaida mtu wa kawaida anaposafiri kwa kutumia ndege kunakuwa hakuna vitu vingi vya kuhofia kwani ni mara chache vitu hivyo huhitajika kubebwa. Mbali na hapo utajitafutia matatizo au kuhatarisha usalama wa abiria wenzako. Jumia Travel imeona ni vema kukutahadhirisha kwamba kutokana na kuongezeka kwa matukio ya kutishia usalama kupitia usafiri huo, hatua kali zimekuwa zikichukuliwa na nchi mbalimbali duniani.

Comments