Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mheshimiwa Balozi Benedict Mashiba wakati alipokutana naye Ofisini kwake Magogoni jijini Dar es salaam leo Jumatano,( Agosti 16, 2017).
…………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mheshimiwa Balozi Benedict Mashiba, ambapo amemtaka kuimarisha mahusiano baina ya nchi zote mbili.
Amekutana na Balozi Mashiba leo (Jumatano, Agosti 16, 2017) katika makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam, ambapo amemtaka balozi huyo kuhakikisha anaboresha shughuli za Kidiplomasia kati ya Tanzania na Malawi.
Pia Waziri Mkuu amemtaka Balozi huyo kuhakikisha anatangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, ukiwemo mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo nchini hususan katika sekta ya viwanda.
Waziri Mkuu amesema licha ya kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii pia amemtaka kuboresha biashara baina ya Tanzania na Malawi kwa kutumia meli mbili za mizigo za Mv. Ruvuma na Mv. Njombe alizozizindua hivi karibuni.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amemtaka Balozi Mashiba kukutana na kufanya mazungumzo na Watanzania waishio nchini Malawi na kuwasisiza kuishi kwa kuzingatia sheria za nchi husika. Pia kuwaunganisha pamoja na kuwashauri waje kuwekeza nchini.
Kwa upande wake Balozi Mashiba amesema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuboresha ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi.
Comments