RAZA AMWAGA ZAWADI MICHEZO YA MASKULI MIKOA


Mwenyekiti wa ZAT ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mhe. Mohammedraza Hassanali akimkabidhi kalkuleta Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Omar Ali Bhai kwa ajili ya washindi wa mashindano ya mpira wa miguu kwa skuli za mikoa yote ya Unguja na Pemba inayotarajiwa kuanza Septemba 12, 2017 katika uwanja wa Amaan Mjni Unguja. 
Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni Hassan Khairalla Tawakal akitoa shukurani kwa Mhe. Raza kwa msaada alioutoa kuwazawadia washindi wa michuano ya mpira wa miguu kwa skuli za mikoa ya Zanzibar itakayofanyika mwezi ujao mjini Zanzibar.Picha na Makame Mshenga.
Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Hassan Khairalla Tawakal, akimtambulisha Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi wa wizara hiyo Omar Ali Bhai kwa Mwenyekiti wa kampuni ya ZAT Mhe. Mohammedraza Hassanali.

Na Salum Vuai, MAELEZO

MKURUGENZI wa kampuni ya usafiri wa anga na huduma za viwanja vya ndege Zanzibar (ZAT) Mohammedraza Hassanali, ametoa wito kwa kampuni na taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi za serikali kuimarisha michezo maskulini.

Akizungungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vitu mbalimbali kwa ajili ya zawadi za washindi kwenye mashindano ya mpira wa miguu mikoa ya Unguja na Pemba iliyofanyika nyumbani kwake Kibweni, Raza alisema ni wajibu wa kila Mzanzibari kusaidia sekta ya michezo.

Alifahamisha kuwa, iwapo wafanyabiashara wa Zanzibar wataunganisha nguvu kwa lengo la kuinua michezo kuanzia ngazi ya skuli ambako ndiko kwenye msingi wa vipaji vizuri, nchi hii itafika mbali kimichezo na kulitangaza vyema jina la Zanzibar. 

“Hii ninchi yetu sote, tuna wajibu kusaidia juhudi za serikali, na nimpongeze Mhe. Rais kwa kuteua Mkurugenzi makini na mwenye jitihada kuongoza Idara ya Michezo na Utamaduni,” alieleza Raza.

Raza ambaye pia ni Mwakilishi wa jimbo la Uzini, alisema hatachoka kutoa msukumo katika sekta ya michezo na misaada mingine ya kijamii, na vitu hivyo alivyotoa ni kutimiza ahadi yake aliyoitoa kabla mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi huyo alikabidhi vityu mbalimbali kwa Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Omar Ali Bai kwa ajili ya zawadi za washindi na washirikiwenmgine wa mashndano hayo yaliyopangwa kuanza Septemba 12, 2017 katika uwanja wa Amaan.

Mkurugenzi Bai aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa wizara yake Bi. Khadija Bakari Juma, akimshukuru Mhe. Raza, alisema kuwekeza katika michezo maskulini ni jambo muhimu kwa kuinua ufahamu wa wanafunzi masomoni.

Alisema dhana za watu wanaodhani mchezo inarejesha nyuma maendeleo ya masomo sio sahihi, kwani ushahidi duniani unaonesha wanafunzi wengine mahodari wamekuwa wakijikita kucheza michezo mbalimbali.

“Akili nzuri hutoka kwenye mwili wenye afya ambao kujengeka kwake kunatokana na mtu kujishughulisha katika michezo ambayo wataalamu wanasema ni sehemu bora kwa makuzi ya watoto”, alieleza.

Alimuahidi mfadhili huyo kwamba vitu vyote alivyovitoa vitafika kwa walengwa, huku akiwaomba wananchi wengine wenye uwezo, makampuni na wafanyabsiahara mbalimbali kushirikiana ili Zanzibar irejeshe hadhi yake michezoni ambayo kwa miaka ya karibuni imeonekana kutetereka.

Mapema, Mkurugenzi wa Idara ya Michezo na Utamaduni katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, alimshukuru Raza kwa moyo wake wa uzalendo, na kuwa tayari kutumia mali zake katika kujenga ustawi wa nchi.

Alisema kuwa Rais Dk. Shein amepania kwa dhati kuendeleza michezo kama anavyofanya katika mambo mengine, na akamsifu Raza kwa kuwa kiungo kizuri kati ya idara yake wanafunzi na watu wengine katika kuhakikisha michezo nchini inapiga hatua. 

Katika hafla hiyo, Raza alikabidhi kalkuleta za kisasa, madishi ya kuhifadhia chakula na kalamu huku akiahidi kufanya mambo mengine makubwa kwa ajili ya kuwashajiisha washiriki wa mashindano hayo ya mikoa sita ya Unguja na Pemba.

Comments