Thursday, August 11, 2011

Wasomalia hawawezi kusubiri tena


Mwandishi Maalum, New York

Balozi Augustine Mahiga, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, ameliambia Baraza Kuu la Usalama kwamba wananchi wa Somalia ambao wanakabiliwa na baa la njaa na ukame hawawezi kuendelea kusubiri tena.

Akizungumza kwa njia ya video teleconference kutokea Mogadishu jana Mahiga alisema zinahitajika dola za kimarekani Bilioni Moja ili kukabiliana na janga hilo la njaa na ukame.

Mahiga aliwataka wajumbe wa Baraza hilo, kuzichagiza serikali zao zichangie kwa haraka na kwa kiwango cha kuridhisha misaada ya kibinadamu kwa mamilioni ya wananchi wa Somalia.

Hata hivyo anasema, hadi wakati anazungumza na Baraza hilo, fedha au michango ambayo imekwisha tolewa na jumuia ya kimataifa ilikuwa haijafikia hata nusu ya mahitajio halisi.

“ Ninawaomba nyie wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama, mzihamasishe serikali zenu zichangie kwa haraka na kuokoa maisha ya wasomali. Kwa ujumla niseme wasomali hawawezi kuendelea kusubiri zaidi” akasema Mahiga.
Balozi Mahiga anasema hali ni ya kutisha, watu wanapoteza maisha kwa idadi kubwa na hasa watoto wadogo.
Akizungumzia hali ya kisiasa na kiusalama na hasa baada ya wapiganaji wa Al Shabaab kuondoka mjini Mogadishu. Mahiga anasema kuondoka kwa kundi hilo kumetoa fursa lakini na changamoto pia.
“Kuondoka kwao kwa kweli ni mshango mkubwa kwetu sote. Na kumetoa changamoto na fursa pia. Fursa ya kwamba sasa Serikali ya Mpito ( TFG) kwa kushirikiana na Vikosi ya Kulinda Amani ( AMISOM)sasa wanashikilia asilimia 95 ya mji wa Mogadishu kwa mara ya kwanza. Changamoto ni namna ya kuendelea kuyashikilia maeneo hayo yaliyoachwa na kundi hilo”. anasisitiza Mahiga.
Anasema, kwa kuimarisha eneo lililoachwa na Al Shabaab kutasaida pia katika kulizuia kundi hilo lisireje tena katika maeneo ambako limeondoka.
Akabainisha kuwa baada ya kundi hilo kurudi nyuma na kutokomea katika maeneo tofauti na likiwa limegawanyika katika mkundi mawili, kumeongeza kasi ya usambazaji wa misaada ya kibanadamu kwa waathirika.
Na kwamba wananchi wengi waliokuwa wakiishi maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na kundi hilo, sasa wanakimbili mjini Mogadishu kutafuta chakula.
Akasema Ofisi ya kisiasa ambayo pia iko chini yake inaendelea kujipanga kwa kufanya tathmini na uchambuzi wa mahitaji halisi ambayo siyo tu yataviwezesha AMISOM na TFG kukalia maeneo yaliyoachwa na Al-Shabaab , bali kuchukua maeneo mengine zaidi na hivyo kupanua wigo wake.
Wakati huo huo Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Bi Susan Rice amesema serikali yake inaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Somalia, Balozi Augustine Mahiga.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa Baraza Kuu. Susan Rice alisema serikali yake imekuwa ikifuatilia kwa karibu kazi nzuri na kubwa inayofanywa na Balozi Mahiga nchini Somalia . Pamoja na vikosi vya kulinda amani vya Afrika na kwamba inaunga mkono kila hatua ya juhudi hizo.
Akabainisha kuwa Marekani, nchi ambayo kwa sasa ndiyo inayoongoza kwa kutoka misaada katika Pembe ya Afrika.Itaendelea kuchangia kwa hali na mali ikiwamo misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Somalia. Pamoja na jitihada za kurejesha amani ya kudumu katika taifa hilo.

No comments: