Afrika Mashariki watakiwa kuchukua hatua biashara ya mihadarati



NAIBU katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) anayeshughulikia shirikisho la kisiasa, Beatrice Kiraso (pichani), ametaka nchi wanachama kuchukua hatua za haraka kukabiliana na biashara haramu ya mihadarati na usafirishaji wa binadamu.
Ametoa kauli hiyo kufuatia kuongezeka kwa takwimu zinazoashiria kuwa nchi za Afrika Mashariki zimeanza kuwa njia kuu za kufanikisha biashara hizo.
Akiwahutubia wakuu wa majeshi ya polisi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ofisa mwandamizi huyo wa EAC alisema nchi wanachama lazima zichukue hatua za makusudi kukabiliana na uhalifu huo.
Alisema kwa kukabiliana na uhalifu huo nchi wanachama zitakuwa zimebaki kuwa salama kwa maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji.
"Biashara hii ya mihadarati na binadamu haituweki katika nafasi nzuri kama kweli tunataka kushawishi uwekezaji zaidi katika utalii na shughuli nyingine za uzalishaji,’’ alisema wakati akifungua mkutano huo Juzi mjini Arusha.
Alizitaka nchi wanachama kuunganisha nguvu zao kukabiliana na uhalifu huo unaotishia amani.
Ili kufanikisha uchunguzi wa kisayansi , ofisa huyo mtendaji wa ngazi za juu ameshauri kuanzishwa kwa kituo kikubwa cha maabara ya uchunguzi katika jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wataalamu kutoka Ujerumani, alisema, wapo tayari kutia shime katika juhudi hizo.
Ofisa huyo pia amesema kwamba ni vyema kukamilisha mkataba kati ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kubadilishana wafungwa na wahalifu kwa manufaa ya EAC.
"Shambulio la kigaidi lililotokea Kampala Julai 2010 ni funzo kubwa kwetu, hali ambayo inatukumbusha haja ya kuwa na mkataba huo," alisema Kiraso katika hotuba yake ambayo Shirika la Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) inayo.

Comments