Sunday, August 28, 2011

Maelfu ya watu wakwama Kilombero, Ulanga

MV Kilombero (ii), MV Kilombero - II, MV kilombero II, MV Kilombero

Baadhi ya abiria wakitoka katika kivuko cha MV Kilombero II upande wa wilaya ya Kilombero wakitokea upande wa wilaya ya Ulanga. (Picha zote na Venance George)
MAELFU ya watu na zaidi ya magari 300 yamekwama kwenye kivuko cha mto Kilombero, mkoani Morogoro, kwa siku tatu sasa kufuatia vivuko viwili vinavyotoa huduma mtoni hapo cha Mv Kilombero I na Mv Kilombero II kupata hitilafu.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Evarist Ndikilo, alisema vivuko hivyo vimepata hitilafu kufuatia kina cha maji kupungua na kusababisha kukita chini kwenye gati ya upande wa Wilaya ya Ulanga.
Ingawa jitihada za kufukua mchanga hufanywa mara kwa mara kuviwezesha vivuko hivyo kuengeshwa, lakini hatua hiyo imetafsiriwa kuchangia vivuko hivyo kugonga kwenye gati na kusababisha hitilafu.
Ndikilo alisema kivuko cha Mv Kilombero II kilipata hitilafu ya kupasuka moja ya injini zake Agosti 26, hivyo kulazimika kusitisha safari.
Alisema kwa vile mto huo kuna vivuko viwili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omar Chambo, aliagiza kivuko cha zamani cha Mv Kilombero I kuanza kufanya kazi mara moja, huku Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) akiagizwa kuanza kukifanyia matengenezo kivuko kilichoharibika.
Hata hivyo, Ndikilo alisema kivuko cha zamani nacho jana kilipata hitilafu ya kutoboka moja ya matangi ya hewa na kuanza kuingiza maji, hali aliyodai ingeweza kuleta hatari kwa abiria na mali zao.
“Pia, tuliona kivuko hicho nacho kisimamishwe ili kifanyiwe matengenezo hayo ya dharura, ikiwamo kurekebisha mbao zilizojengwa kwenye kivuko hicho, ambazo zimekuwa zikileta usumbufu na kuhatarisha maisha ya abiria,” alisema.
Ndikilo alisisitiza kuwa Tamesa chini ya Chambo ambaye alifika eneo la tukio jana, imechukua hatua za dharura kufungua injini iliyopasuka ya Mv Kilombero II na inatarajiwa kupelekwa Mang’ula ili kuchomelewa.
Pia, alisema Serikali imejipanga kuleta injini mpya inayotarajiwa kuwasili Kilombero kati ya wiki moja au mbili zijazo, ili kuziba pengo la injini iliyoharibika.
“Matengenezo tutakayoyafanya pale Mang’ula ni ya dharura tu, kuwezesha huduma zisisimame kwa muda mrefu, tuna matumaini baada ya injini hiyo kurekebishwa itarejeshwa na kufungwa kwenye kivuko ndani ya siku chache zijazo,” alisema.
Aliwaomba wananchi na wasafiri wanaotumia vivuko vya mto huo kuwa wavumilivu kwa madai kuwa, kutokea kwa hitilafu kama hiyo ni jambo la kawaida kutokana na vifaa hivyo kuwa ni vyombo vya moto. Habari hii imeandikwa na
Venance George wa Mwananchi Morogoro




No comments: