Wingu zito lazidi kutanda UDA



Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Deo Filikunjombe akiwaonyesha waandishi wa habari jinsi Idi Simba alivyoingiziwa Sh 250milioni katika akaunti yake ikiwa malipo ya kuuza hisa za Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), mjini Dodoma jana.

Habel Chidawali, Dodoma
WINGU zito bado limeugubika mkataba wa uuzwaji wa hisa za Serikali ndani ya Shirila la Usafiri Dar es Salaam (Uda), kufuatia wanaodai kuwa wamiliki wake kujitokeza hadharani tangu kuanza kwa mvutano ambao umekuwa ukizihusisha pande tofauti.

Wamiliki hao ni Kampuni ya Simon Group Ltd ambao jana waliwambia waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa umiliki wake umekidhi vigezo vyote katika kumiliki Hisa kwa asilimia 52.53.

Hata hivyo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) jana hiyohiyo ilirusha kombora na kusema kuwa mkataba huo ni batili na kwamba fedha zote zipo kwenye akaunti ya kada wa Chama Cha Mapinduzi na mwanasiasa wa siku nyingi (jina tunalihifadhi kwa sasa).

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Simon Group, Robert Kisera alisema kampuni yake ilifuata vigezo vyote vilivyotakiwa na kwamba imejidhatiti kuliendesha Uda bila wasiwasi.

Kisera alisema kuwa hadi sasa kampuni yake imekwishawekeza kiasi cha Sh760 milioni na kwamba kiasi kilichobaki cha Sh500 kinatarajia kulipwa kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Msimamo wa POAC
Kwa upande wake, Mwenyekiti POAC, Zitto Kabwe aliitisha mkutano wa Waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge na kueleza kuwa mkataba wa Uda na Simon ni kizungumkuti na kutahadharisha kuwa aliyeingia mkataba huo amejiingiza matatani mwenyewe.

Zitto alisema kuwa kilichofanyika ndani ya mkataba huo ni ufisadi mtupu na akaeleza kuwa tayari kamati yake ilishabaini kuwa yako madudu makubwa hivyo ikaomba Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuingilia kati kwa ajili ya kufanya ukaguzi kwa kina.
“Taratibu hazikufuatwa,na uamuzi wowote utakaofanyika ni batili kwa kuwa tayari sisi tumeshaanza mchakato wa kubaini kilichopo ndani ya mkataba huo ikiwa ni pamoja kumuagiza CAG na tayari Spika ana taarifa hizo,’’alisema Zitto.

“Kutokana na hilo, hapa jamaa kaingia choo cha kike na kwa vyovyote vile lazima ametapeliwa na wajanja kwa kuwa kamati ilishamwambia mapema lakini anashindwa kuelewa kuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma ndiyo yenye jukumu la kubinafsisha mashirika zaidi ya hapo ni hakuna.’’

Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Deo Filikunjombe (Ludewa-CCM) alisema kuwa kinachoyatafuna mashirika ya umma ni Msajili wa Hazina ambaye ameshindwa kutimiza wajibu wake kwa zaidi ya miaka 10.

Filikunjombe alisema kuwa kwa zaidi ya Miaka 10 Msajili ameshindwa kuteua bodi jambo linaloonyesha kuwa uwezo wake ni mdogo sana ambao hata kwa dawa asingeweza kujinusuru zaidi ya kusababisha migogoro kila kunapokucha.

Alisema kutokuwapo kwa bodi kulifanya uamuzi kufanyika kiholela holela jambo ambalo limeifanya Kamati hiyo kuwa na shaka.Mbunge huyo alisema kuwa kuna uzembe ndani ya serikali ambao umekuwa ukisababisha baadhi ya wachache kuendelea kutafuna mali za umma wakati nchi ikibaki maskini.

“Kwa mfano angalieni tarehe hizi 2/9/2009 ziliingia Sh 250,00 milioni ziliingia Benki M’, Makambako tarehe 26/11/2009 ziliingizwa Sh 20 milioni Benk M’ Songea kabla ya tarehe 9/12/2009 kuingizwa kiasi cha Sh 30 milioni katika tawi la Mlimani City zote zikiwa ni akaunti za (anamtaja mwanasiasa huyo),".

Alisema kumekuwapo maneno ya kuichafua kamati hiyo kwamba inafanya kazi chini ya mwamvuli wa vigogo walioko ndani ya Serikali jambo alilokanusha.

“Kwanza Watanzania naomba watambue kuwa Simon haijanunua Uda, bali kilichopo ni kwamba Simon ilinunua zile hisa ambazo hazikuwa zimelipiwa na kuwa hakuna kigogo yeyote nyuma ya kampuni hii na huyo wanayemtaja mimi simfahamu," alisema Kisera.

Shutuma nyingi alizirusha kwa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ambaye alisema kuwa kuwa ndiye amekuwa akiichafua Simon Group na kumtaka mbunge huyo kufunga mdomo ili asiingilie mambo yoyote kuhusu mkataba huo.Kwa mujibu wa Kisera, kitendo cha Mnyika kuandika barua kwenye ukusara wa ‘face book’ akielekeza shutuma kwa Simon ni kitendo cha uonevu na manyanyaso kwa mwekezaji mzawa.

Mnyika aliingilia kati mvutano ulioko kati ya Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi na Meneja wa Uda, Victor Milanzi, akisema hakuna mwenye haki ya kumnyooshea mwingine kidole, kwani wote wawili ni sehemu ya matatizo yanayolikabili shirika hilo.

“…Wote wawili wameshiriki kwa kiwango kikubwa katika kukiuka sheria, kanuni na taratibu kwenye uendeshaji wa Uda bila kuzingatia kwa ukamilifu maslahi ya wasafiri na walipa kodi,” alisema Mnyika katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa kupitia mtandao wa face book.


SOURCE:Mwananchi

Comments