Mbowe: Tutakwenda sote Ofisi za Manispaa na tutalala pale



Jioni ya leo hapa jijini Arusha ambapo Mweyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Freeman Mbowe amesema kuwepo madarakani hadi 2015 kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ni haki kikatiba, lakini akaonya kuwa umma unaweza kuamua vinginevyo iwapo Serikali itashindwa kuongoza kwa kujibu mahitaji na maslahi ya jamii.

Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya NMC eneo la Unga Ltd mjini hapa alisema chama chake kinataka amani na ufumbuzi wa kudumu kuhusu tatizo la umeya Arusha ili kuruhusu shughuli za maendeleo na kiuchumi ziendelee kwa kufanyika mazungumzo ya haki na yenye nia njema kwa maslahi ya umma badala ya vyama kama ambavyo CCM kimekuwa ikifanya kuhusu mgogoro huo.

“Amani itapatikana kwa kutenda haki. Amani haiwezi kupatikana kwa kauli za viongozi au vitisho. Tumekubaliana na Waziri Mkuu siku 30 kumaliza mgogoro wa Umeya Arusha, baada hapo tutakwenda sote Ofisi za Manispaa na tutalala pale hadi kieleweke,” alisema Mbowe.

Alisema uamuzi wa kuwatimua madiwani ulikuwa mgumu na ulifikiwa usiku wa manane katika kikao kilichoanza Saa 3:00 asubuhi baada ya wahusika kukataa kusikiliza ushauri wa watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini waliowataka kutekeleza maagizo ya Kamati Kuu.

Naye Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema yeye na chama chake wapo tayari kufanya maandamano nchi nzima kutoka Mwanza hadi Ikulu ya Magogoni Dar es Salaam kumuomba Rais Jakaya Kikwete kuachia madaraka, iwapo ameshindwa kuhimili nguvu ya umma inayotaka mabadiliko na utatuzi wa matatizo kadhaa yanayoikabili taifa.

Tishio hilo la Dk Slaa linakuja miezi michache baada ya Rais Kikwete kuhutubia taifa mnamo mwezi na kueleza kwambaba, maandamano ya Chadema katika kona mbalimbali nchini yalikuwa na dhamira ya kutaka kuingia madarakani kwa mabavu licha ya kumalizika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Alitishia kufanya maandamano ya nchi nzima ambayo atayaongoza kuanzia Mwanza hadi Ikulu ya Magogoni Dar es Salaam kumuomba Rais Kikwete kuachia madaraka kutokana na taifa kukabiliwa na matatizo mengi huku yeye akiwa ameshindwa kuyatatua.


Wenje

Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje na mwenzake wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa walisema wananchi wa majimbo yao wanaunga mkono uamuzi wa kuwatimua madiwani wasaliti huku Msigwa akienda mbali zaidi kwa kusema kila mapinduzi hutengeneza mashujaa na wasaliti wake.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu, Lazaro Maasai alimuonya Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha kuwa ataongoza wananchi wa Arusha kumfungia nje iwapo ataendelea kuwatambua na kuwaruhusu madiwani waliofukuzwa uanachama.

Comments