Mahalu awataja Mkapa, Kikwete mahakamani


Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia Prof Costa Mahalu akiangalia vielelezo vyake vya ushahidi katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana,kabla ya kutoa ushahidi na kesi yake ya kuhujumu uchumi na kuisababishia hasara Serikali zaidi ya sh Bilioni 2,kuahilishwa hadi tarehe 26 mwezi huu.Picha na Michael Jamson

ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameieleza Mahakama kuwa alimtaarifu Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kuhusu hali ya ofisi ya ubalozi ilivyokuwa mbaya.

Mahalu na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin, wanakabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi na kuisababishia Serikali, hasara ya zaidi ya Sh2bilioni wakati wa ununuzi wa jengo la ofisi za ubalozi wa Tanzania mjini Rome, Italia.

Jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahalu alitumia zaidi ya saa tatu kujitetea huku baadhi ya utetezi wake ukitawaliwa na kukataliwa kwa baadhi ya nyaraka alizoziwalisha kama ushahidi.

Akiongozwa na wakili wake, Mabere Marando, Mahalu alidai kuwa mwaka 2001 wakati Mkapa alipokwenda Brussels nchini Ubelgiji, alionana naye na kumtaarifu kuhusu hali ya ofisi za ubalozi huo kuwa mbaya.

“Mwezi Mei mwaka 2001, nilitaarifiwa kuwa Mkapa atakwenda Ubelgiji na mimi nilimwomba Katibu Mkuu wangu, Balozi Kibelo aniruhusu nikamweleze juu ya matatizo yaliyokuwa kwenye ofisi yetu,"alidai Mahalu na kuongeza:

“Nilionana na Rais Mkapa na aliniambia anafahamu suala hilo kwa kuwa ofisi za ubalozi huo, zilikuwa zimefungwa kwa muda mrefu hivyo aliniambia atajitahidi kupata fedha za kujenga ama kununua jengo lenye hadhi za ofisi za ubalozi.”

Mkapa ni mmoja wa mashahidi wa upande wa utetezi ambaye tayari aliwasilisha utetezi wake wa maandishi ulioandaliwa kwa njia ya kiapo kumtetea Profesa Mahalu.
Kwa mujibu wa kiapo chake kilichowasilishwa mahakamani hapo, Mkapa anadai kuwa jengo la ofisi ya ubalozi mjini Rome, lilinunuliwa wakati ambao yeye akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alidai kwamba ununuzi wa jengo hilo ulifanyika kwa mujibu wa sera ya Serikali ya kumiliki au kujenga ofisi za kudumu na makazi kwa mabalozi nje ya Tanzania ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza gharama kwa Serikali.

Maelezo zaidi ya Mahalu
Mahalu alidai kuwa baada ya kuonana na Mkapa, alimjulisha Balozi Kibelo juu ya mazungumzo yao na kwamba alimuahidi kuwa atalifuatilia na kulipeleka katika bajeti ya wizara husika.
Alidai kuwa masuala yote ya fedha yalikuwa yakiletwa kwake, lakini alikuwa hayashughulikii moja kwa moja kwa sababu chini yake kulikuwa na mhasibu.
SOURCE :MWANANCHI

Comments