Monday, August 08, 2011

Ajali yaua diwani


ALIYEKUWA Diwani wa kata ya Hai Mjini Mkoani Kilimanjaro Ombaeli Lema (37) pamoja na mkewe Rachel Uronu (35) wamefariki dunia katika ajali ya gari.

Ajali hiyo iliyotokea katika barabara kuu ya Sanya Juu, Bomang’ombe katika maeneo ya Kwa Mose kijiji cha Mungushi ilihusisha magari mawili aina ya Fuso na Toyota Pick up yaliyogongana uso kwa uso.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Absalomu Mwakyoma ajali hiyo ilitokea Agosti saba mwaka huu, majira ya saa tatu usiku katika kijiji cha Mungushi Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Alisema katika ajali hiyo lori la mizigo aina ya Fuso lenye namba T 279 ACL lilikuwa likiendeshwa na Hezekieli Mwafifi liligongana na gari dogo aina ya Toyota Pick Up lenye namba za usajili T954 AFU lililokuwa likiendeshwa na marehemu Ombaeli Lema.

Alisema gari hilo dogo, lililokuwa na Diwani pamoja na mkewe waliokuwa wametoka nyumbani kwa wazazi wao katika kijiji cha Ivaeny maeneo ya Kibong’oto na walikuwa wakirejea nyumbani kwao maeneo ya Bomang’ombe Wilayani Hai.

Alisema gari aina Fuso lililokuwa likielekea Sanya Juu lilipofika eneo la tukio ndipo lilipogongana na gari hilo dogo na kusababisha vifo vya wanafamilia hao.

Kwa mujibu wa taarifa toka kwa Kamanda alisema Ombaeli Lema alifia papo hapo na mkewe alifariki mara baada ya kufikishwa katika hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi

Hata hivyo kamanda huyo alisema kuwa dereva wa lori anashikiliwa na Jeshi na polisi huku upelelezi zaidi ukiendelea na mwili wa marehemu Ombaeli Lema umehifadhiwa katika hospitali Kibong’oto huku mwili wa mkewe Rachel umehifadhiwa katika hospitali ya KCMC. SOURCE: MWANANCHI

No comments: