Monday, August 08, 2011

Warembo Miss Tanzania waanza kambi rasmi

Warembo wanaowania taji la Vodacom Miss Tanzania 2011, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuwasili katika kambi yao iliyopo Hotel ya Giraffe Ocean View Mbezi Beach jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Mpigapicha Wetu).
Mkuu wa Udhamini wa Vodacom Tanzania, George Rwehumbiza akizungumza na warembo wanaowania taji la Miss Tanzania 2011, baada ya kuwasili katika kambi yao iliyopo Hotel ya Giraffe Ocean View Mbezi Beach jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Mpigapicha Wetu).

Mwandishi Wetu

JUMLA ya warembo 30 kutoka kanda tofauti nchini leo wameanza rasmi kambi ya Vodacom Miss Tanzania 2011 yaliyopangwa kufanyika Septemba 10 kwenye ukumbi wa Mlimani City kwa mfumo tofauti na ule uliozoeleka miaka ya nyuma ambapo warembo walikuwa wakikaa kambini katika Hotel ya Giraffe iliyopo jijini Dar es Salaam.

Vodacom Tanzania ambao ndio wadhamamini wakuu wa shindano la Vodacom Miss Tanzania kwa miaka kadhaa mfululizo safari hii wamebadilisha kabisa muundo wa awali na hivyo walimbwende hao watakaa ndani ya jumba maalum lililopewa jina ‘Vodacom House’.

Mkuu wa Udhamini wa kampuni hiyo George Rwehumbiza amesema jijini Dar es Salaam kuwa lengo la kufikiwa kwa mabadiliko hayo ni kulifanya shindano hilo liwe na muonekano tofauti kama ilivyo kwa Vodacom ambayo imebadili muonekano wake na kasi ya utoaji huduma.

“Safari hii warembo 30 wanaoshiriki shindano hili la Vodacom Miss Tanzania wataishi kwenye jumba maalum ‘Vodacom House’ na humo watafundishwa vitu mbalimbali ikiwemo jinsi ya kukabiliana na vishawishi hususan katika masuala ya kimapenzi,” alisema Rwehumbiza.

Akitaja malengo mengine ya kuwaweka washiriki hao ndani ya jumba hilo Mkuu huyo wa udhamini alisema kampuni yake kwa sasa inatoa huduma kwa teknolojia yenye kasi zaidi hivyo warembo hawana budi kuendana nayo kwa kufundishwa aina ya kula, kuondoa ulimbukeni mara wanapopata umaarufu.

Mabadiliko haya yatalifanya shindano hili kuwa bora na linaloenda na wakati kama zilivyo huduma zetu yaliyotokana na mabadiliko ya nembo yetu. Wakiwa ndani ya jumba warembo watakaa kwa wiki tatu wakijifunza masuala ya kijamii, alisema Rwehumbiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Lino Agency waandaaji wa shindano hilo Hashim Lundenga amesema kwa mwaka huu wanataka warembo wenye sifa ikiwemo elimu, muonekano na tabia nzuri ili mshindi atakayepatikana aweze kutuwakilisha vema katika medani za kimataifa.

“Sisi hatuangalii mshiriki ametoka wapi iwe kijijini au mjini, tunachozingatia ni mrembo kukidhi viwango vya shindano ikiwemo sifa tunazozitaka ili mwisho wa siku kila mtu ajivunie mafanikio aliyoyapata akiwa ndani ya jumba la Vodacom House na atumie kigezo hicho kufanikiwa kimaisha,” alisema Lundenga.

Lundenga alisema kuwa mfumo wa mashindano ya mwaka huu, umebadilika ambapo jumla ya warembo 15 wataingia hatua ya nusu fainali baadala ya 10 kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Alisema kuwa kati ya warembo hao 10, watano watapatikana katika mashindano maalum wakiwa katika Vodacom House. Kwa mujibu wa Lundenga, kutakuwa na mashindano ya Top Model ambayo yatafanyika leo na baadaye kufuatiwa na mashindano ya Vipaji (Talent), Mrembo bora wa muonekano katika picha (Miss Photogenic), Mrembo bora wa michezo (Top Sports Woman) na mrembo atakayeonyesha ushirikiano mkubwa na uchangamfu katika kambi, Miss Personality.

Ili kuishirikisha jamii, maisha ya washiriki hao wa Vodacom Miss Tanzania 2011 ndani ya Vodacom House yatakuwa yakioneshwa moja kwa moja ‘Live’ na vituo vya Startv pamoja na Clouds TV ili kutoa nafasi kwa watazamaji kumpigia kura mrembo anayefaa kuvikwa taji hilo na kumrithi Genevieve Mpangala mshindi anayemaliza muda wake.


No comments: