Thursday, August 18, 2011

Grand Malt yazindua chupa ya mililita 330


KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Grand Malt imezindua chupa mpya ya aina yake yenye ujazo wa mililita 330 katika kiwanda chake cha Dar es Salaam jana.

Kinywaji hicho, ambacho hakina kilevi kwa sasa kinauzwa kwenye kopo zenye ujazo wa mililita 330 lakini kuanzia leo kitapatikana kwenye chupa mpya itakayouzwa Sh1,000 kwa chupa na Sh 20,000 kwa kasha kwa bei ya reja reja.

“Chupa hii mpya itaziba pengo katika soko na kukifanya kinywaji hiki kupatikana kwa urahisi,” alisema Mkurugenzi wa Masoko wa TBL David Minja huku akisisitiza kuwa kinwaji hicho bado kitapatikana kwenye kopo pia.

Alisema Grand Malt ilizinduliwa Aprili mwaka jana lakini kwa sasa ni kinywaji namba moja kisichokuwa na kilevi Tanzania. “Tunawashukuru sana wateja wetu na umma kwa ujumla kwa kukikubali kinywaji hiki na kukifanya kiwe namba moja. Tunawahakikishia kuwa kitakuwepo sokoni muda wote ili kuendelea kuwaburudisha watanzania,” alisema Minja.

“Tunapozindua kinywaji hiki leo, tunapenda kuwahakikishia wateja wetu kuwa kinywaji kitakachouzwa kwenye chupa ni sawa na kile ambacho kinauzwa kwenye kopo, ambacho kina vitamini na mchanganyiko wa maziwa ya aina yake,” alisema Minja.

Meneja wa Grand Malt Consolata Adam alisema, “Grand Malt ilizinduliwa Tanzania mwaka jana na leo tunapozindua chupa hii mpya, tunawashukuru wateja wetu kwa kutuunga mkono.”

Alisema kinywaji hicho kimetokea kuwa bora kwa sababu ya ladha yake nzuri inayoifanya inyweke kirahisi kwa kuwa ina vitamini, laktosi yenye ladha nzuri, inayoitofautisha na malt zingine sokoni.

“Kinywaji hiki kinawafaa wafanyakazi wenye shughuli nyingi lakini pia kinafaa kwa matumizi ya nyumbani, wafanyakazi wa usiku, wanafunzi, vikao vya kibiashara na sherehe nyinginezo,” alisema Bi Consolata.

Alisema TBL itaendelea kukitangaza na kusambaza kinwaji hiki na kuhakikisha kinawafikia watanzania wengi zaidi popote walipo.

No comments: