KAMPALA, Uganda
JULIUS Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania, Juni mosi atatangazwa rasmi na Waganda kuwa Mtakatifu, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra ya kukumbuka Siku ya Mashahidi wa Dini.
Taarifa kutoka nchini Uganda zimeeleza kwamba baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika na mjane wa Nyerere, Mama Maria Nyerere pia watahudhuria sherehe hizo zinazotarajiwa kufanyika huko Namugongo nchini Uganda.
Mwaka jana, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alishiriki katika kampeni za kutaka Nyerere, ambaye serikali yake ya awamu ya kwanza iliongoza vita vya kuundoa utawala wa kijeshi wa Uganda, atangazwe kuwa mtakatifu.
Kampeni hizo zilianza mwaka 2006 baada ya Vatican kukubali ombi lililowasilishwa na askofu wa Jimbo la Musoma lililo kaskazini mwa Tanzania.
Maandalizi ya sherehe hiyo yanaendelea kwa kiwango cha juu na msimamizi wa shughuli hiyo, Padri Dennis Ssebuggwawo alisema shamrashamra hizo zitatanguliwa na siku tisa za maombi maalum, zitakazoanza Mei 26 na kuisha Juni 2.
Alisema jimbo la Moroto ndiyo litakakuwa mwenyeji wa sherehe hizo mwaka huu na zitakazoongozwa na neno lenye kichwa cha habari “Nipo pamoja nanyi siku zote hata ukamilifu wa dahari (Mathayo28:20)".
Mashahidi 22 wa dini wa Kanisa Katoliki waliuawa kati ya mwaka 1885 na 1886.
Hata hivyo, rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec), Askofu Yuda Thadei Ruwa’ichi amesema kuwa hatua hiyo ni upotoshaji wa makusudi na si sahihi. SOURCE; NEWVISION UGANDA & MWANANCHI
Comments