Liyumba apatikana na hatia, ahukumiwa kwenda jela miaka miwili!
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo imesoma Hukumu dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Amatus Liyumba,Katika hukumu hiyo Liyumba amepatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela miaka miwili dhidi ya kesi ya utumiaji mmbaya wa madaraka .
Hukumu hiyo imetolewa muda mfupi uliyopita baada ya kumuona mtuhumiwa ana kosa la kutumia vibaya madaraka na hivyo kustahili kwenda jela. Hata hivyo, wakili wa mtuhumiwa, Majura Magafu, hakuridhika na hukumu hiyo kwa madai kuwa kuna makosa mengi ya kisheria yamefanyika hivyo anakata rufaa na kwamba taratibu za kutimiza rufaa hiyo, zinaanza leo leo.
Wakati wote wa kusomwa kwa hukumu hiyo, Liyumba alionekana kutokwa jasho na hivyo shati lake lote kuloa. Hali mahakamani hapo ilikuwa tete kutokana na kugawika kwa mitizamo ya watu, wapo walioona hakutendewa haki na wengine kusema miaka miwili ni midogo ukilinganisha na uzito wa tuhuma alizokuwa akikabiliwa nazo. Picha zaidi za tukio zitawajia baadae kidogo....
===================
Awali Liyumba alifikishwa mahakamani hapo akiwa pamoja na aliyekuwa meneja miradi wa BoT Deogratius Kweka, ambapo kwa pamoja walikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kutumia vibaya madaraka aliyokuwa nayo, jambo lililopelekea serikali kupata hasala ya sh bilioni 221, kupitia ujenzi wa majengo pacha ya BoT.
Hata hivyo kabla ya kuanza kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, upande wa mashtaka ulimuachia aliyekuwa mshtakiwa mwenza wa Liyumba {Kweka}, na kumshitaki Liyumba kwa kesi hiyo.Upande huo wa mashtaka uliita mahakamani hapo mashahidi 8, wakiwamo waliokuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa BoT, pamoja na kutoa vielelezo mbali mbali vinavyohusiana na kesi hiyo.
Baada ya ushahidi huo kumalika kusikilizwa, Mahakama ilifikia uamuzi wa kumfutia Liyumba shtaka la kuisababishia serikali hasala ya bilioni 221 baada ya Upande huo wa serikali kupitia ushahidi na vielelezo vyake kushindwa kuithibitishia mahakama hiyo kama Liyumba alihusika na kosa hilo.Kufuatia uamuzi huo, mahakama ilimtaka Liyumba kujitetea juu ya uhusika wake katika shtaka la kutumia vibaya madaraka aliyokuwa nayo.
Katika utetezi wake Liyumba alijitetea mwenyewe kama shahidi wa kwanza kutoka upande wa utetezi, na baadae alimwiita shahidi wa pili ambaye ni Bosco Ndimbo Kimela, aliyekuwa katibu wa BoT.Baada ya kumaliza usikilizwaji wa ushahidi huo, mahakam hiyo ilizitaka pande zote mbili kuwasilisha hoja zao za kisheria, ambapo alipanga kusoma hukumu dhidi ya Liyumba ifikapo May 24, 2010.
source: michuzi blog
Comments