Tuesday, May 25, 2010

JK ahisi ahisi hatari EAC



MWENYEKITI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Jakaya Kikwete ametaka viongozi na wanajumuiya wa Umoja huo kuepuka kuchukua hatua au kutoa matamko yatakayochokoza mataifa jingine wanachama au viongozi na watu wake kwani kufanya hivyo kutahatarisha umoja.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana alipohutubuia Bunge la jumuia hiyo mjini Nairobi Kenya katika mkutano wa tatu wa Bunge hilo.

“Ninawataka viongozi wote wa Afrika Mashariki, waandishi wa habari, watu wenye ushawishi katika jamii, wachambuzi wa masuala mbalimbali ya jamii, kuepuka kuchukua hatua au kutoa kauli ambazo zitachokoza taifa, viongozi na au watu wake,” alisema Rais Kikwete.

Alisema vitendo hivyo vitavuruga uelewano imani iliyoanza kujijenga miongoni mwao, ambalo ni jambo muhimu kwa ushirikiano huo wa kikanda.

“Haya masuala ndiyo yanayoharibu imani iliyokuwapo, ambayo ni muhimu kwa mafanikio ya ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ni lazima tutambue maneno na uchokozi ndivyo vilivyoisambaratisha jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977,”alisema.

Alisema kukosekana kwa imani miongoni mwa mataifa wanachama ndiko kulikoiporomosha jumuiya ya mwanzo ya Afrika Mashariki hivyo akataka kutorejewa tena makosa ya awali.

“Ni lazima tujizuie kurudia makosa tuliyoyafanya awali. Najua, kutaibuka tofauti miongoni mwetu, lakini hebu basi tutafute njia muafaka za kukabiliana nazo. Ni lazima tuepuke kutoa matamko ya uchokozi dhidi ya wengine hadharani, hii itavuruga kuaminiana na kuua moyo uliojengwa wa kiudugu na kushirikiana,”alisema.

Alisema ni lazima mataifa hayo wanachama yafahamu kuwa hakuna ushirikiano unaweza kusonga mbele kukiwa na mazingira mabaya ya kutoaminiana na kupoteza imani miongoni mwao. SOURCE: HOTUBA YA RAIS.

No comments: