DC ajeruhiwa katika fumanizi

MKUU wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha ameumizwa vibaya kichwani baada ya kushambuliwa sehemu mbali mbali za mwili wake  na kusukumwa katika fumanizi lililotokea katika hoteli ya Angorn Arms Mjini Songea.

Akizungumza na Mwananchi jana wakati wa kikao cha kwanza cha kamati ya mkoa  ya usimamizi wa pembejeo  Mkuu huyo amesema, tukio hilo limetokea jana usiku majira ya saa nne wakati akiwa katika chumbani alichopanga  no 102 katika hoteli hiyo alivamiwa na kundi la watu wakiwemo waandishi wa habari na kumtaka afungue mlango na alipofungua walianza kumpiga na kumvua nguo na kumwacha akiwa uchi wa mnyama huku wakimpiga picha za utupu.

Anasema, chanzo cha tukio hilo ambalo yeye ameliita ni la ujambazi ni wivu uliotokana na mwandishi mmoja wa habari kukataliwa, anasema akiwa chumbani humo na mwanamke ambaye anadaiwa kuwa naye ni mwanahabari alishitukia akipigwa na kuvuliwa nguo.
Alisema, katika vurugu hizo amepoteza pesa taslimu Sh laki mbili, simu ya mkononi aina ya Nokia namba N78 yenye thamani ya shilingi laki tano pamoja na pete yake ya ndoa.

"Tukio hilo limetokana na wivu kwani kuna mwandishi wa habari niliwahi kuwa na mahusiano naye siku za nyuma na baada ya kumwacha ameingiwa na wivu na kuamua kunifanyia vurugu hata hivyo nimesharipoti tukio hilo katika vyombo vya usalama nasubiri   hatua za kisheria zifuate mkondo wake,"alisema DC huyo.

Alisema watu hao walimshambulia  kwa makusudi na hawakufata taratibu zozote za uongozi wa hoteli, wala kumchukua mwenyekiti wa serikali za mtaa ndiyo maana analichukulia swala hilo kama ni ujambazi kwani wamefanyia ukatili kuingia katika chumba chake na kumshambulia.Habari ya Joyce Joliga, Songea.

Comments