Wednesday, September 02, 2009

Zain yajiunga mkongo wa mawasiliano na Seacom


Zain Tanzania imekuwa kampuni ya kwanza ya simu za mkononi kujiunga na mkonga wa baharini wa kimataifa ambao utaiwezesha Tanzania na eneo la Afrika Mashariki kupata huduma za data za kasi zaidi na yenye gharama nafuu.

SEACOM ina uwezo mkubwa wa kubeba na kuunganisha huduma za sauti na data ukilinganisha na mfumo wa satellite uliozoeleka. ‘’Wateja wetu watarajie kupata huduma za kasi zaidi za intaneti, huduma bora zaidi za simu za sauti, kasi katika kuunganishwa na uwezo mkubwa wa kupokea huduma za data,’’ alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Zain Tanzania.

‘’Uhusiano wa moja kwa moja wa huduma ya Zain ya 3.5G na SEACOM itawawezesha wateja wetu kupata huduma ya kasi ya intaneti kupitia simu za mkononi na uwezo mkubwa wa kupokea data kutoka vituo vikuu vya data duniani.

Hii ni hatua ya maendeleo kwa Zain na tunajivuna kwamba tunaendelea kuweka historia nchini Tanzania kwa kuwa kampuni ya kwanza ya simu za mkononi kuleta huduma hii iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu, na yakutegemewa kwa wateja wetu, sekta ya biashara na taasisi za elimu,’’ alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Zain Tanzania.

Mkonga huu ni wa kwanza katika miradi ya mikonga ya baharini Afrika Mashariki ambao utaiunganisha Tanzania na dunia, Licha ya maendeleo katika sekta ya habari na mawasiliano ya teknolojia Afrika katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, bara la Afrika bado lina matumizi madogo ya simu na intaneti.

Maendeleo ya kiuchumi Afrika Mashariki na Afrika Kusini pia yamecheleweshwa na bei kubwa ya teknolojia ya mawasiliano na habari na miundo mbinu hafifu ya mawasiliano. Mahitaji ya huduma za data katika bara la Afrika yamekuwa yakizidi huduma iliyopo kwa sasa, na mkonga utasaidi kukuza biashara nchini Tanzania na katika bara hili, alisema Khaled.

No comments: