Utata waibuka kesi ya Mramba, Yona



MAWAKILI upande wa utetezi katika kesi ya kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh 11 bilioni, inayomkabili Waziri wa zamani wa Wizara ya Fedha, Basil Mramba na wenzake, wamekana kuutambua waraka namba mbili wa mwaka 1999 wa aliyekuwa Jaji Mkuu, Francis Nyarali.

Jopo hilo, la mawakili liliukataa waraka huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam mbele ya jopo la mahakimu watatu, lililokuwa likongozwa na Hakimu, John Lutamwa wakati kesi hiyo, ilipokuja kwa ajili ya usikilizaji wa awali.

Mawakili hao, waliukataa waraka namba mbili wa mwaka 1999 ambao unautaka upande wa utetezi kutaja idadi ya mashahidi wao kabla ya upande wa mashtaka kuanza kutoa ushahidi wao na mahakama kuthibitisha kama washtakiwa wana hatia au la, kwa madai kuwa ulitengenezwa kinyume cha sheria.

Wakili wa Mramba, Hurbert Nyange alidai kwa heshima na taadhima kifungu cha sheria cha 192, kifungu kidogo cha nne cha mwenendo wa kesi za jinai, mwenye mamlaka ya kutengeneza taratibu za kisheria ni Waziri wa Sheria akishauriana na Jaji Mkuu.

“Ni rai yangu kuwa sheria yoyote ambayo imetengenezwa chini ya kifungu hiki, lazima itangazwe kwenye gazeti la serikali," alidai Nyange.

Alidai waraka huo, hauonyeshi ni lini utaanza kutumika na kwamba kama kweli hiyo ni sheria haikutengenezwa chini ya mamlaka husika.

Alidai anaiheshimu nafasi ya jaji mkuu ya kutoa miongozo ya sheria kuhusiana na mienendo ya kesi na kwamba kama wakili na ofisa wa mahakama anawajibu wa kufikia maamuzi kwa misingi ya kisheria.

“Kwa heshima kubwa mbele ya mahakama nimeangalia karatasi ya Mei 5,1999 ambayo ni ya Jaji Mkuu, mwisho nikaona haina saini ya aliyekuwa Jaji Mkuu marehemu Francis Nyarali hivyo nina wasiwasi nayo,” alidai Nyange.

Alidai kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 231 cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai mtuhumiwa anapaswa kueleza idadi ya mashahidi wake hadi hapo upande wa mashtaka utakapofungua kesi yao na mahakama kumuona ana hatia.

Comments