Darasa la saba kufanya mitihani leo



WANAFUNZI 1,026,806 kote nchini kesho wanaanza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi utakaofanyika kwa siku mbili, huku kukiwa na upungufu wa asilimia 1.9 kulinganisha na mwaka uliopita.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa idadi hiyo ni pungufu ya wanafunzi watahiniwa 20,394 waliofanya mtihani huo mwaka jana.
Waziri Mahiza alisema katika idadi hiyo, wavulana ni 511,840 na wasichana 514,966, idadi ambayo ni pungufu ya wavulana 6522 na wasichana ni 13872 ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2008.
Alisema kati ya watahiniwa wa mwaka huu, watahiniwa 13,819 watafanya mtihani huo kwa lugha ya Kiingereza kutokana na kusoma katika shule ambazo zinaendesha mafunzo yake kwa lugha hiyo na kwamba watahiniwa wengine watafanya kwa lugha ya Kiswahili.
Mheshimiwa Mahiza alisema kuwa kati ya wanafunzi waliosajiliwa wapo wa elimu maalumu ambao ni pamoja na wanafunzi 164 wenye matatizo ya kuona na ambao wanahitaji maandishi makubwa. Kati ya wanafunzi hao wenye matatizo ya kuona, 93 ni wavulana na 71 ni wasichana. Gedius Rwiza na Makoba Hassan

Comments