RAIS Jakaya Kikwete kesho ataanza staili mpya ya kuwasiliana moja kwa moja na wananchi wakati atakaposikiliza hoja, kujibu maswali na kupata maoni yao juu ya mustakabali wa nchi, Ikulu imesema jana.
Kikwete, ambaye alizungumza na taifa kwa mara ya mwisho Juni 11 alipozungumza na wazee wa mkoani Dodoma, atafanya mazungumzo hayo ya dakika 90 kwa njia ya televisheni kuanzia saa 2:30 usiku wakati atakapopokea simu na kusikiliza maswali, ushauri, maoni na kujibu moja kwa moja.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais inaeleza kuwa katika staili hiyo ya aina yake, Rais Kikwete pia atapokea ushauri kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu (sms) kutoka kwa watazamaji na ujumbe wa barua pepe, ikiwa ni mpango wa kusikiliza matarajio ya wananchi katika jitihada zao za kuboresha maisha yao kwa kujiletea maendeleo.
"Rais atatumia aina mpya ya kuwasiliana na wananchi kwa kusikiliza hoja zao, kwa kujibu maswali yao, kusikiliza ushauri wao na kupata maoni juu ya mambo yanayohusu mustakabali wa nchi yetu, serikali yetu na maendeleo yetu," inaeleza taarifa hiyo.
"Mazungumzo hayo yatakachukua muda wa dakika 90 kuanzia saa mbili unusu usiku (saa 2:30 usiku) hadi saa nne kamili usiku."
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chini ya mpango huo rais atazungumza moja kwa moja kupitia vituo vya redio na televisheni vya Shirika la Utangazaji (TBC) na vyombo vingine vya utangazaji nchini.
Kurugenzi hiyo ya Mawasiliano Ikulu, ilifafanua kwamba "mbali na TBC, televisheni nyingine za ITV, TVZ, Mlimani TV, Tumaini TV na Channel Ten zinatarajiwa kuonyesha mazungumzo hayo".
Taarifa ya kurugenzi hiyo imevitaja vituo vitakavyotangaza moja kwa moja mazungumzo hayo kuwa ni TBC-Taifa, Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), Radio Mlimani, Radio Clouds, Radio Tumaini, na Radio Uhuru.
Ikulu pia imetaja namba zitakazotumika kwa ajili ya maswali, maoni, hoja, ushauri utakaotolewa moja kwa moja kupitia TBC. Namba hizo ni +255-22-2772448, +255-22-2772452 na +255-22-2772454.
Pia kwa watakaotaka kutuma ujumbe mfupi wa simu watatakiwa kutuma kwenda namba 0788-500019, 0714-591589 na 0764-807683, huku wale watakaotaka kutumia barua pepe watatuma kwenda anuani ya swalikwarais@yahoo.com.
Comments