Monday, September 28, 2009

Wanafunzi Kibasila watoa kali ya mwaka





ZAIDI ya wanafunzi 2,600 wa Shule ya Sekondari ya Kibasila jijini Dar es Salaam jana walifunga barabara za Mandela na Chang’ombe kwa zaidi ya saa tano na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.

Wanafunzi hao waliendesha operesheni hiyo kuzuia magari kupita baada ya kukaa kwenye makutano ya barabara hizo mbili, wakiishinikiza serikali iweke matuta eneo hilo ambalo limekuwa na ajali nyingi tangu Barabara ya Mandela ifunguliwe kiasi cha kupachikwa jina la Machinjioni.

Ajali hizo, zikiwemo zilizotokea mwishoni mwa wiki iliyopita, zimekuwa zikichukua roho za watu wengi, na hasa wanafunzi wa shule hiyo inayopakana kwa upande mmoja na Barabara ya Mandela na upande mwingine Barabara ya Chang’ombe.

Wanafunzi hao walifunga barabara hiyo kuanzia saa 3:00 asubuhi na magari ambayo yalijaribu kupita kwa nguvu yalirushiwa mawe na vioo vya baadhi ya magari vilivunjwa.

Wakati wakiendelea kuyarushia mawe magari hayo, baadhi walikuwa wakiimba nyimbo za kutaka Mkuu wa Mkoa, William Lukuvi aende eneo hilo na kutoa ufumbuzi wa haraka kuhusu ajali hizo.

"Hatudanganyiki, tunamtaka mkuu wa mkoa," walisikika wanafunzi hao wakiimba.

No comments: