Tuesday, June 09, 2009

Deci balaa jipya lazuka


WAKATI Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo anatarajiwa kutoa taarifa mbele ya Bunge kuhusu Taasisi ya Upatu ya Deci, jana polisi walilazimika kutumia mtutu wa bunduki kuwatawanya wanachama waliovamia ofisi za makao makuu ya taasisi hiyo, zilizopo Mabibo, jijini Dar es Salaam na kufanya vurugu wakidai kurejeshewa fedha zao.

Vurugu hizo zililipuka baada ya mmoja wa wafanyakazi wa Deci kuwaeleza wanachama hao kuwa tamko la kurejeshewa fedha zao litatolewa kwenye mkutano wa Bunge ulioanza jana mjini Dodoma.

Ijumaa iliyopita Mkurugenzi Mtendaji wa Deci, Timothy Ole Loitingy’e aliwaeleza wanachama wao waliokuwa wamekusanyika katika ofisi hizo, kuwa tume iliyoundwa kuichunguza taasisi hiyo itatoa tamko jana, hivyo kuwataka wanachama hao kutawanyika; nao wakafanya hivyo baada ya kuridhika na maelezo hayo.

Tofauti na matarajio yao, wanachama hao walipofika jana katika ofisi hizo hakukuwa na kiongozi hata mmoja wa taasisi hiyo zaidi ya walinzi, wafanyakazi pamoja na askari polisi waliokuwa wanalinda eneo hilo.

Sakata hilo lilianza baada ya mmoja wa wafanyakazi wa Deci kuwaeleza wanachama hao kuwa, tume haijatoa tamko lolote na kuwataka wanachama kufuatilia mkutano wa Bunge kwa sababu tamko juu ya taasisi hiyo litatolewa bungeni.

Juzi Waziri Mkulo alisema kuwa, atatoa tamko hilo ndani ya saa 48, ikimaanisha kuwa wakati wowote leo atatangaza hatima ya taasisi hiyo pamoja na malipo ya wanachama wake.

Baada ya kauli ya mfanyakazi huyo wa Deci ambaye hakutaja jina lake, wanachama hao walianza kuyavamia magari mawili yaliyokuwa nje ya ofisi hizo na kuyavunja vioo huku wakitishia kuyachoma moto. Taarifa ni ya Fidelis Butahe na Simon Simalenga Kwa habari zaidi kuhusiana na Deci hebu soma hapa upate habari hizi kwa kina.

No comments: