Friday, June 12, 2009

Balozi mpya wa Marekani nchini


Rais Obama amteua Alfonso Lenhardt (pichani) kuwa Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Rais Barack Obama amemteua Mheshimiwa Alfonso E. Lenhardt kuwa Balozi wake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mujibu wa mfumo unaotumiwa na Serikali ya Marekani, Rais huteua Mabalozi kwa mashauriano na hatimaye kupata ridhaa ya Bunge la Seneti la Marekani.

Toka Mwezi Mei 2004, Mheshimiwa Lenhardt amekuwa Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Kuzuia Uhalifu (National Crime Prevention Council - NCPC) ambalo ni taasisi isiyo ya Kiserikali na isiyozalisha faida. Pia alikuwa Makamu wa Rais wa Kundi la Makampuni ya Shaw akishughulikia Uhusiano na Serikali. Tarehe 4 Septemba 2001 aliteuliwa kuwa Mpambe wa Bunge (Sergeant-at-Arms) wa 36 wa Bunge la Seneti la Marekani na kuwa Muamerika wa Kwanza mwenye asili ya Kiafrika kuhudumu katika wadhifa huo ndani ya Bunge la Marekani. Aidha, alihudumu kama Makamu wa Rais na Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Baraza linaloshughulikia Wakfu Mbalimbali (Council on Foundations).

Mheshimiwa Lenhardt alistaafu kutoka katika Jeshi la Marekani hapo August 1997 akiwa na cheo cha Meja Jenerali, baada ya kulitumikia jeshi hilo kwa zaidi ya miaka 30 katika ngazi mbalimbali za uongozi. Wadhifa wake wa mwisho jeshini ulikuwa ni Mkuu wa Kamandi ya Uajiri, yenye makao makuu yake huko,Fort Knox, KY, ambao aliongoza na kusimamia taasisi iliyojumuisha zaidi ya watu 13,000 waliokuwa katika zaidi ya vituo vya kazi 1,800. Aidha, aliwahi kudumu kama Afisa Mwandamizi wa Polisi Jeshi (Senior Military Police Officer) katika oparesheni zote za kipolisi na masuala ya usalama katika Jeshi la Marekani sehemu mbalimbali duniani.

Mheshimiwa Lenhardt ambaye alizaliwa katika jiji la New York, ana Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Sheria kuhusu Makosa ya Jinai kutoka katika Chuo Kikuu cha Nebraska, Shahada ya Pili ya Sanaa Katika Utawala kutoka katika Chuo Kikuu cha Central Michigan na Shahada ya Pili ya Sayansi ya Utawala katika Sheria kutoka katika Chuo Kikuu cha Serikali cha Wichita. Aidha, Mheshimiwa Lenhardt ni mhitimu wa awamu ya 94 Katika Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo ya Usalama cha FBI; programu ya Viongozi wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai ya Jeshi la Marekani . Aidha ni mhitimu wa Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo ya Kivita (the National War College) na Chuo Kikuu cha Mambo ya Kijeshi na Usalama (National Defence University).

Kuhusu Uteuzi wa Mheshimiwa Lenhardt na mabalozi wengine, Rais Obama alisema, "Wamarekani watafaidika sana kwa kuwa na watumishi hawa waliotukuka, wake kwa waume, kama wawakilishi wao nchi za nje. Vipaji, uzoefu na kujitoa kwao kikamilifu kutakuwa na mchango mkubwa sana tunapoendelea kuimarisha ubia kati ya Marekani na mataifa mbalimbali duniani kote na kukabiliana na changamoto kubwa za karne ya 21. Ninashukuru kwa utumishi wao na nina shauku kubwa ya kufanya kazi na kila mmoja wao."

Kwa taarifa zaidi kuhusu tangazo la uteuzi huu kutoka Ikulu ya Marekani tembelea tovuti: http://www.whitehouse.gov/the_press_office/President-Obama-Announces-More-Key-Administration-Posts-6-11-09/

No comments: