RAIS Jakaya Kikwete ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Vyombo vya Usafiri wa Majini na nchi Kavu (Sumatra) kuongeza udhibiti wa usalama wa vyombo vya majini ili kupunguza ajali zisizo na ulazima zinazotokea majini.
Rais Kikwete alisema hayo wakati alipokuwa akizindua rasmi mradi wa kivuko cha MV Magogoni kilichoundwa kwa gharama ya Sh 8.5 bilioni na chenye uwezo wa kubeba tani 500 wakiwemo abiria 2,000 na magari 60.
“Nawaagiza nyinyi Sumatra hakikisheni kwamba vyombo vya majini vinakaguliwa mara kwa mara ili kupunguza ajali hizi zisizo na lazima, msifanye fujo mnapotuona sisi, lakini tukiondoka mnachezea maisha ya watu,”alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa Sumatra wanastahili kulaumiwa kuhusiana na matukio ya vifo yanayotokea majini kwa ajili ya uzembe wa wataalamu wao wa kutokuwa makini katika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vyombo hivyo jambo ambalo husababisha majonzi na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi wanaotumia usafiri wa majini.
Rais Kikwete alisema uchakavu wa vyombo vya majini umeendea kuleta majonzi makubwa katika jamii kutokana na uzembe wa watu wachache , hivyo ni vema ukawepo utaratibu utakaoonyesha wazembe kazini ili waweze kuchukuliwa hatua za makusudi kabisa.
Alisema serikali kupitia nchi wahisani tayari ipo katika mchakato wa kuhakikisha kuwa ujenzi wa daraja la litakalounganisha wakazi wa Kigamboni unaanza mapema mwakani kwa lengo la kupisha fursa za uwekezaji maendeleo.
Comments