Tuesday, June 02, 2009

Jitihada Kuitafuta Ndege ya Ufaransa zaendelea


Jitihada za kuitafuta ndege ya abiria ya Ufaransa, Air France AF447 ambayo ilipotea baada ya kupoteza mawasiliano na rada ikiwa na abiria 228, zinaendelea kaskazini kwa Brazili ingawa kuna matumaini finyu ya kumpata mtu atakayenusurika. Ndege hiyo kubwa ya abiria aina ya Airbus A330 ikiwa na abiria 228 ilikuwa ikitoka Rio de Janeiro, Brazili kuelekea Paris, Ufaransa wakati ilipopoteza mawasiliano ya rada masaa manne baada ya kuruka toka uwanja wa ndege wa Rio de Janeiro.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba mtoto mchanga mmoja, watoto saba, wanawake 82 na wanaume 126.
Asilimia kubwa ya abiria wengi waliokuwemo kwenye ndege hiyo inasemekana ni raia wa Brazili.
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy alisema kwamba kuna matumaini madogo sana ya kumpata mtu atakayenusurika kwenye ajali hiyo.
Ndege hiyo ilikumbwa na hali mbaya ya hewa iliyoambatana na radi masaa manne baada ya kupaa.
Dakika 15 baada ya ndege hiyo kupigwa na radi ujumbe uliokuwa ukijulisha hitilafu ya umeme katika ndege hiyo ulipatikana.
Baada ya hapo ndege hiyo ilipoteza mawasiliano kabisa na rada kwa masaa kadhaa na kuhofiwa kwamba itakuwa imeanguka kwenye bahari ya Atlantic karibu na pwani ya Brazili.
Ndege tano za jeshi la Brazili na helikopta mbili zilikuwa zikitafuta mabaki ya ndege hiyo kwenye eneo la kilomita 1100 kaskazini mwa Brazili.
Hata hivyo jeshi la Brazili lilibidi lisimamishe kwa muda jitihada za kuitafuta ndege hiyo kutokana na hali mbaya ya hewa.
Meli za kijeshi za Brazili zinategemewa kuongeza nguvu ya kutafuta mabaki ya ndege hiyo ingawa zitachelewa kidogo kufika eneo la tukio.

No comments: