Wanajeshi waongezewa umri wa kustaafu


AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya ikwete ameongeza umri wa kustaafu kwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania(JWTZ) kulingana na ngazi zao kutoka miaka 57 hadi 60.

Mabadiliko hayo mengine ni kwamba, makao makuu ya jeshi hilo ndio yatakuwa yanashughulikia majukumu ya kisera na yale ya kulinda amani yatakuwa chini ya komandi.

Kauli ilitolewa jana na Rais Kikwete mara baada ya kuzindua Komandi ya Jeshi la Nchi Kavu(LFC) katika Kambi ya Nyerere iliyopo eneo la Msangani, Kibaha mikoani Pwani.


“Uzinduzi wa komandi hiyo ni ushahidi kuwa jeshi liko tayari na kwenda na wakati kiutendaji na kiutaalamu. Pia nimekubali kuongeza umri wa kustaafu kwa wanajeshi wa ngazi za juu kuwa miaka 60 badala ya 57,” alisema Kikwete.

Rais Kikweti aliliomba jeshi hilo kuendelea kuwa wabunifu ili kujenga uwiano wa kiutendaji pamoja na kulitaka kufanya mabadiliko zaidi kwa kuangalia muundo wake, mitaala na vifaa ilivyonavyo pia viende na wakati.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono na itajitahidi kuwapa upendeleo maalum.

Aliwapongeza wanajeshi kwa kulinda uhuru na mipaka ya nchi kwa kipindi cha miaka 45 tangu lilipoanzishwa. Alitoa mfano katika kipindhi hichi limeshiriki katika operesheni nyingi duniani kuanzia ile ya mwaka
1978 ya Uganda, mapambano ya ukombozi kumekucha ya mwaka 1960, Safisha Msumbiji 1986-1988 na ya Anjuan.

Rais Kikwete alisema jeshi hilo sasa linashiriki katika vikosi vya Umoja wa Matiafa vya kulinda amani nchini Lebanon.

“Sasa tunajiandaa kupeleka wanajeshi Darfur na pia hivi karibuni tumepokea maombi ya kupeleka wanajeshi Chad…,” alisema.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi alisema wizara yake itaendelea kushughulikia kero na changamoto mbali mbali za wanajeshi kulingana na uwezo wa kifedha.

Comments