Wednesday, March 04, 2009

Salva na mkanganyiko wa maelezo Ikulu

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

GAZETI la Mwananchi la leo, Jumatano, Machi 4, 2009 limeandika habari zenye kichwa cha habari: “Kikwete ajitosa sakata la umeme” kikifuatiwa na habari iliyoonyesha kuwa Mhe. Rais amejiingiza katika suala la ununuzi wa mitambo ya umeme ya Dowans.

Mwananchi limeandika habari hiyo, kama ilivyofanywa na vyombo vingine vyote vya habari, kutokana na taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais kufuatia kikao cha jana cha tathmini ya utendaji wa Serikali kati ya Rais Kikwete na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake.

Vyombo vingine vyote vimeripoti habari hii kwa usahihi kama ilivyotolewa.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais inapenda kuwaarifu wananchi kuwa gazeti la Mwananchi limesema uongo kwa kupindisha ukweli na kupotosha habari iliyotolewa. Huu ni upotoshaji wa makusudi ambao shabaha yake inajulikana kwa gazeti la Mwananchi peke yake. Ni uchochezi tu wa kumwingiza Mhe. Rais katika suala ambalo hahusiki nalo kabisa. Suala la Dowans halikujadiliwa kabisa katika kikao cha jana.

Kwa hakika, ni ukosefu mkubwa wa heshima kwa chombo chochote cha habari kumlisha maneno Rais wa nchi likijua kuwa maneno hayo siyo ya kweli kama Mwananchi lenyewe linavyokiri katika habari yake.

Katika aya yake ya pili ya habari hiyo, Mwananchi linasema na ninanukuu: “Lakini taarifa kuhusu makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha ufuatiliaji baina ya Rais Kikwete na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake, haikutaja mitambo ya Dowans kuwa ni sehemu ya mambo yaliyojadiliwa.”

Sasa kama Mwananchi linajua ukweli kuwa suala la Dowans halikujadiliwa katika kikao hicho, limepata wapi habari za kumhusisha Rais na suala zima la mitambo ya umeme ya Dowans?

Jibu ni rahisi. Hili ni gazeti ambalo limeanza kubobea katika kutunga na kupindisha habari zinazohusu Serikali na shughuli za Mhe Rais. Limeanza kubobea katika kuwapotosha kwa makusudi wananchi kwa malengo ambayo yanajulikana kwa gazeti lenyewe. Limebobea katika kuichokonoa Serikali kwa kupindisha ukweli ulio wazi.

Mifano michache ifuatayo inatosha kuthibitisha ukweli huo:

(a) Jumatano, Januari 21, mwaka huu, 2009, Toleo Namba 03145 la gazeti hilo liliandika kichwa cha habari kikisema kuwa “Ikulu ilichukua faili la Kagoda” wakati likijua kuwa siyo kweli.

(b) Ijumaa, Januari 23, mwaka huu, 2009, Toleo Namba 03147 la gazeti hilo liliandika habari yenye kichwa cha habari: “Kikwete achafua hali ya siasa Zanzibar” likijua kuwa hiyo siyo kweli.

(c) Jumamosi, Januari 24, mwaka huu, 2009, Toleo Namba 03148 la gazeti hilo liliandika, miongoni mwa mambo mengine, na nanukuu “Kikwete anamaanisha Serikali itaendelea kuwekwa na wao…Wazanzibar hawana haki ya kujichagulia Rais wanayemtaka, bali CCM na Serikali ndiyo itawachagulia Rais wa kuwaongoza.. basi sasa tusubiri tuone.” Kauli hii inalenga dhahiri kujenga chuki miongoni mwa wananchi wa Zanzibar dhidi ya Rais Kikwete na Serikali ya Muungano.

(d) Katika hotuba ya Salamu za Mwaka Mpya kwa Wananchi iliyotolewa Desemba 31, mwaka jana, 2008, Rais alisisitiza umuhimu wa kulinda amani na utulivu wa Tanzania. Hata hivyo, ukweli huo haukulizuia gazeti hilo la Ijumaa, Januari 2, mwaka huu, 2009 Toleo Namba 03126 kukariri wapinzani wakisema kuwa tadhahari hiyo ilikuwa ni vitisho, wakati likijua dhahiri kuwa hilo siyo kweli.

Kurugenzi ya Mawasilianao ya Rais inapenda, kwa mara nyingine, kusisitiza kuwa uandishi wa upotoshaji na kupindisha ukweli ni hadaa kwa wananchi.

Serikali ya Mhe. Kikwete itaendelea kuheshimu na kuimarisha uhuru wa habari nchini. Lakini pia ni matarajio ya Serikali kwamba vyombo vyetu vya habari vitakijita na kuongozwa na maadili ya taaaluma yanayosisitiza kuandika habari za kweli na kuepuka uandishi na utangazaji wa habari unaokiuka maadili ya taaluma yenyewe ya uandishi wa habari.
Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

04 Machi, 2009 soma majibu ya utumbo wa huyu jamaa hapa http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=10449

2 comments:

Anonymous said...

heading yako ni nzuri, salva na mkanganyiko wa maelezo ikulu, hujasema anajikakanganya vipi,tafadhari wafuatiliaji someni maelezo ya gazeti la mwananchi kujibu mkanganyiko huo. salva anasikitisha, anapelekwa na siasa zaid kuliko kazi.
bahati mbaya kumbe alihusika richmond,

Anonymous said...

heading yako ni nzuri, salva na mkanganyiko wa maelezo ikulu, hujasema anajikakanganya vipi,tafadhari wafuatiliaji someni maelezo ya gazeti la mwananchi kujibu mkanganyiko huo. salva anasikitisha, anapelekwa na siasa zaid kuliko kazi.
bahati mbaya kumbe alihusika richmond,