MBUNGE wa Busanda, Faustine Rwilomba (CCM) amefariki dunia akiwa nchini India alikokuwa akitibiwa.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema Rwilomba alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo tangu Desemba mwaka jana.
Kabla ya kwenda kulazwa katika Hospitali ya Indraspratha Appolo, iliyopo Mji wa New Delhi, India, alikuwa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili .
Kwa mujibu wa Dk Kashililah, mwili wa Rwilomba uliwasili jana jioni Dar es Salaam na uko Hospitali ya Jeshi Lugalo.
Heshima za mwisho zitatolewa Jumamosi kabla ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Busanda ,Wilayani Geita, Mkoa wa Mwanza. Katibu huyo wa bunge alisema ratiba kamili ya mazishi itatolewa Machi 13 2009.
Kifo cha mbunge huyo wa CCM kimetokea miezi michache baada ya mbunge mwingine wa chama hicho wa Mbeya Vijijini, Richard Nyaulawa (57) kufariki Novemba mwaka jana.
Rwilomba alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2000 kuwa mbunge wa Busanda na kutetea nafasi hiyo katika uchaguzi wa mkuu wa mwaka 2005.
Comments