Mkutano wa IMF na Afrika waanza





MKUTANO kuhusu mabadiliko ya kiuchumi duniani na jinsi Afrika inavyoweza kukabiliana na changamoto za tatizo hilo ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) umeanza leo ambapo shirika hilo limeonya kuwa mamilioni ya watu watarejea kwenye hali ya umaskini wa kupindukia kutokana na kuanguka kwa kiuchumi duniani, huku Tanzania ikisema itapoteza miradi miwili yenye thamani ya Sh4.7 trilioni kutokana na tatizo hilo.

Kukosekana kwa fedha hizo za uwekezaji katika miradi ya madini ya aluminiam na nikeli, kumekuja wakati tayari sekta nyingine, ikiwemo ya utalii, zikiwa zimepigwa na mawimbi mazito ya kuporomoka kwa uchumi duniani kulikoanzia na msukosuko wa kifedha uliozikumba nchi tajiri.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano kuhusu mabadiliko ya kiuchumi duniani na jinsi Afrika inavyoweza kukabiliana na changamoto za tatizo hilo, mkurugenzi mkuu wa IMF, Dominique Strauss-Kahn alisema uchumi katika mwaka 2009 utaporomoka zaidi na kuwa na maendeleo hasi, akisema kuwa hiyo ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 60.

Strauss-Kahn alisema matatizo yanayoendelea kwenye taasisi za kifedha duniani, pamoja na kupotea kwa imani miongoni mwa walaji na biashara kunafanya mahitaji ndani ya nchi kote duniani kushuka.

Comments