Tuesday, March 03, 2009

Koplo Rashid Lema hoi


HALI ya afya ya Koplo Rashid Lema, mshtakiwa wa 11 katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva wa teksi, jijini Dar es Salaam, inazidi kuwa mbaya na sasa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Koplo Lema ni mmoja wa washtakiwa tisa katika kesi hiyo, akiwemo mshtakiwa namba moja, Abdallah Zombe, ambaye alikuwa mkuu wa upelelezi wa Dar es Salaam na ambaye wakati wa mauaji hayo alikuwa akikaimu nafasi ya Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam.

DC Lema, ambaye ni shahidi muhimu wa utetezi kulingana na maelezo yake ya awali katika kesi hiyo, alilazimika kulazwa hospitalini hapo jana akitokea katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke alikokuwa amelazwa tangu juzi. Kulazwa kwake kulisababisha uvumi kuwa mtuhumiwa huyo amefariki dunia.

Lakini Mwananchi ilimkuta kwenye sehemu ya mapokezi ya Muhimbili majira ya saa 9:20, akiwa amelala kwenye moja ya mabenchi wakati anasubiri huduma, huku akiwa chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Magereza wapatao sita.

Hata hivyo, Koplo Lema, ambaye alionekana kuwa katika hali mbaya, hakuweza kupata huduma mapema wala kupokelewa hadi askari waliokuwa wakimlinda walipowafokea wahudumu wa hospitali hiyo kutokana na kucheleweshewa huduma.

Mmoja wa askari hao, ambaye Mwananchi ilielezwa na askari mwingine kuwa ndiye kiongozi wao, alikuwa akiwafokea wahudumu wa hospitali hiyo alisikika akisema kuwa walimfikisha mgonjwa huyo hospitalini hapo tangu saa 5.30, lakini hadi wakati huo (majira ya saa 9.20) alikuwa bado hajapokelewa.

Baada ya askari hao kufoka kwa nguvu, mmoja wa wahudumu wa kiume wa hospitali hiyo alifika na kumchukua mgonjwa huyo kwenye kiti cha magurudumu akishirikiana na askari hao na kumpeleka wodini.

“Mnatufanya sisi kama wajinga. Tangu tumefika hapa mnatupita na kutuangalia tu bila huduma," alifoka askari huyo. Tumefika hapa tangu saa 5.30, lakini hadi sasa hamjatuhudumia.” Habari hii imendaliwa na James Magai wa Mwananchi.