Monday, March 02, 2009

Rais Guinea Bissau auawa



BISSAU, Guinea-Bissau
WANAJESHI jana walimuua rais wa Guinea-Bissau, Joao Bernado "Nino" Vieira katika tukio linaloonyesha wazi kuwa la kulipiza kisasi lililofanyika saa chache baada ya mkuu wa majeshi wa taifa hilo la Afrika Magharibi kuuawa.
Taarifa zilizopatikana jana, muda mfupi baada ya mauaji hayo zilieleza kuwa Vieira aliuawa akiwa katika makazi yake, siku moja baada ya mlipuko wa bomu kumuua mnadhimu mkuu wa jeshi, Jenerali Batista Tagme Na Wai.

Muda mfupi baada ya kuuawa kwa Rais Vieira, jeshi la nchi hiyo lilitoa taarifa likieleza kuwa hakuna mpango wowote wa mapinduzi ya serikali.

Katika taarifa aliyoitoa kupitia redio na televisheni ya nchi hiyo msemaji wa jeshi, Zamora Induta alithibitisha taarifa za kuuawa kwa rais huyo na kuwa kifo hicho kimesababishwa na kundi dogo la jeshi ambalo bado halijatambulika lakini akadai kwa sasa linasakwa.

Katika kikao cha dharura cha baraza la mawaziri la nchi hiyo, Iduta alisema kuwa viongozi wa juu wa jeshi waliwaeleza viongozi wa serikali kuwa hayo si mapinduzi.

“Tuna msimamo wetu wa kuthamini serikali inayoingia madarkani kidemokrasia pamoja na katiba ya jamhuri yetu. Watu waliomuua Rais Vieira bado hawajakamatwa, lakini tunaendelea na juhudi za kuhakikisha wanapatikana. Ni kundi fulani lililojitenga... kwa sasa kila kitu kimedhibitiwa,” alieleza Induta.

Taarifa hiyo ya jeshi kupitia kwa Induta ilikanusha madai ya awali kuwa Vieira ameuawa katika shambulio la kulipiza kisasi baada ya kuuawa kwa mkuu wa majeshi kwa mlipuko wa bomu jana usiku.

Wawili hao walikuwa wakionekana kuwa wapinzani wakubwa katika masuala ya kisiasa na kikabila na wote wamewahi kunusurika katika majaribio kadhaa ya kuuawa.

Vieira anayetoka katika kabila dogo la Papel aliwahi kuwatuhumu maafisa kutoka katika kabila kubwa la Balanta kwa kutaka kumpindua na baadhi yao waliuawa na wengine kadhaa kufungwa maisha gerezani.

Mmoja miongoni mwao alikuwa Waie, ambaye katika miaka ya themanini alitupwa na kutelekezwa katika kisiwa chenye misitu minene kwenye pwani ya nchi hiyo.

Msaidizi wa Waie, Luteni Kanali Bwam Namtcho alieleza kuwa Waie alitelekezwa kwenye kisiwa hicho kwa miaka kadhaa, kabla ya kurejeshwa na kutangaziwa msamaha na Vieira.

Namtcho alisema kuwa bomu lililomuua Waie juzi lilikuwa limefichwa chini ya ngazi zilizo sehemu ya kuingilia ofisini kwake kwenye makao makuu ya jeshi la nchi hiyo.

No comments: