Saturday, January 05, 2008

Nuru ya urais Marekani yamwelekea Obama


KWA jinsi mambo yanavyokwenda huenda muafrika wa kwanza akaukwaa urais wa Marekani. Seneta Barack Obama, ambaye baba yake ni Mjaluo na mama yake ni mzungu, ameshinda katika uchaguzi wa urais upande wa Democrats huko Iowa. Obama ni mweusi na asilimia 95% ya wananchi wa Iowa ni wazungu. Wiki ijayo New Hampshire watapiga kura zao za awali.

Kwa ushindi huo mkubwa katika hatua ya kwanza ya kinyanganyiro cha kuwania uteuzi wa kuwa mgombea wa kiti cha Urais katika uchaguzi wa Novemba nchini Marekani, kilichoanzia huko IOWA, Mdemocrat Barack Obama amejisafishia njia. Hatua itakayofuata sasa ni kutafuta ridhaa ya wanachama wake katika jimbo la New Hampshire.

Barack Obama aliwaangusha wenzake wa chama chake cha Democrats akimuacha John Edwards nafasi ya pili na Hilary Clinton mke wa rais wa zamani Bill Clinton katika nafasi ya tatu. Hadi matokeo yanatangazwa Obama na Clinton ndiyo waliokua wakitajwa kuwa na ushindani mkubwa huku matumaini ya kuibuka mshindi yakielekezwa kwa bibi Clinton.

Ushindi wa Obama huko Iowa ni hatua ya kwanza katika kiu chake cha kutaka kuwa Rais wa kwanza mweusi katika historia ya Marekani na ametoa changamoto kubwa kwa wapinzani wake wakuu Edwards na Hilary Clinton, kutafakari juu ya mkakati wa kampeni zao kukiwa kumesalia maeneo mengine 28 ya kutafuta ridhaa ya wanachama, kabla ya kuidhinishwa na mkutano mkuu wa chama kuwa mgombea.

Hatua hii ya kwanza Obama mwenye umri wa miaka 46 imezusha mshtuko, wakati hapo kabla alionekana kuwa nyuma ya mpinzani wake mkuu, kwa mujibu wa kura za maoni ya wanachama wa chama chake.

Ubaguzi ulivyokuwa mbaya kuna weusi walisema kuwa hawatampigia kura maana wanahofia kuwa akichaguliwa kuwa rais atauawa na wazungu wabaguzi kama Martin Luther King Jr. na Medgar Evers! Hofu yao si ya kuchekwa maana Obama amepewa ulinzi wa Secret Service mapema kabla ya wagombea wengine. Hiyo ni kwa sababu hao wabaguzi walitishia kumuua.

No comments: