BoT wafanya mabadiliko


KATIKA harakati za kusafisha uozo ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Gavana Profesa Benno Ndulu, amefanya mabadiliko makubwa ndani ya taasisi hiyo nyeti ya fedha nchini kwa kupangua safu ya wakurugenzi wa Idara mbalimbali.

Mabadiliko hayo ambayo ni ya kwanza kufanywa na GAvana Ndulu tangu ateuliwe kushika wadhifa huo wiki iliyopita, yamemng'oa mmoja wa vigogo wa benki hiyo Amatus Liyumba ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi (DPA).

Gavana Profesa Ndulu, alimweleza mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana kuhusu mabadiliko hayo ambaye lengo lake ni kuboresha utendaji ndani ya BoT.

Awali taarifa zilizofikia gazeti hili kutoka vyanzo habari ndani ya serikali, zilisema taarifa za mabadiliko hayo zimetangazwa juzi jioni.

Profesa Ndulu alimtaja Leornad Kasalika kutoka BoT tawi la Arusha kuchukua nafasi ya Liyumba.

Kwa mujibu wa Profesa Ndulu, Liyumba atapangiwa kazi nyingine na kuongeza kwamba mabadiliko hayo yameangalia mambo matatu ya msingi.

Alisema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha mazingira ya utendaji ili kuleta tija na ufanisi ndani ya benki.

Alifafanua kwamba, mabadiliko hayo yamegusa idara karibu zote isipokuwa Idara ya Uchumi, Fedha na Masoko.

Gavana huyo ambaye amekuwa akiangaliwa kama mwenye kuweza kuleta mabadiliko ndani ya BoT kutokana na uzoefu wake wa kufanya kazi Benki ya Dunia (WB) alifahamisha kwamba mabadiliko hayo yamegusa idara za makao makuu na matawi yote ya benki hiyo, isipokuwa Mwanza.

Matawi ya BoT nchini ukiacha Mwanza ni pamoja na Zanzibar, Mbeya na Arusha ambayo yamekuwa yakiongozwa na wakurugenzi huku.

Alizitaja idara nyingine zilizohusika na mabadiliko hayo kuwa ni Fedha, Benki, Idara inayoshughulikia Deni la Taifa na inayoshughulikia Zabuni.

Profesa Ndulu aliongeza kwamba katika mabadiliko hayo, baadhi ya wakurugenzi wamepandishwa, wengine kuondolewa na baadhi kuhamishwa idara.

Hata hivyo, Profesa Ndulu alisema taarifa zaidi kuhusu idara na majina ya watu walioteuliwa zitatangazwa wakati wowote kuanzia sasa.

Ingawa hakutaja majina zaidi, alisema wakurugenzi watano ni wapya ambao wamepandishwa.

Alisema mabadiliko hayo pia yameondoa watu ambao walikaa muda mrefu katika idara zao, kupandisha vijana na kuleta uwiano wa rika la uongozi kwa kuzingatia sifa zinazostahili.

Mabadiliko hayo ya wakurugenzi yamefanywa siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kumfukuza kazi Ballali na kuagiza kuwa watu wote waliohusika katika ufisadi wa Sh133 bilioni katika Akaunti ya Mabdeni ya Nje (EPA) katika ya benki hiyo washughulikiwe mara moja.

Hatua hiyo pia imekuja huku Kikosi Kazi (Task Force) kinachoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Johnson Mwanyika, kikiwa kimepewa miezi sita kuhakikisha wote waliohusika kuanzia ndani ya BoT na wamiliki wa makampuni 22 wanachunguzwa na kukamatwa kisha kufikishwa katika vyombo vya sheria na fedha zirejesheshwe. Habari hii imeandikwa na Ramadhan Semtawa wa Mwananchi

Comments

Anonymous said…
Naona mabadiliko ni hatua nzuri kwa BoT.Na gavanampongeza