Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amewakaribisha waandaaji wa kipindi cha “Safari Field Challenge” kuhamishia mashindano hayo katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa msimu ujao, akieleza kuwa hatua hiyo itatoa fursa ya kutangaza zaidi vivutio vya utalii vilivyopo Kusini mwa Tanzania.
Amesema Hifadhi ya Ruaha inakuwa sahihi kwani kupitia Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kumefanyika maboresho makubwa ya hifadhi hiyo ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege, vituo vya kutolea taarifa, maeneo ya kupumzika pamoja na nyumba za kulala wageni.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo Novemba 28, 2026 wakati wa hafla ya fainali za “Safari Field Challenge”, ambapo amewapongeza waandaaji kwa ubunifu na juhudi zao za kuendeleza taaluma ya uongozaji watalii nchini.
Amesema waongoza watalii ni wadau muhimu katika sekta ya utalii kwa kuwa wanakutana moja kwa moja na watalii na hivyo kuwa mabalozi wakuu wa Tanzania, vivutio vyake na utamaduni wake kwa wageni wanaokuja nchini.
Katika mashindano hayo, Felix Mpelembwa ameibuka mshindi wa kwanza na kutambuliwa kuwa Muongozaji Bora wa Watalii Tanzania, huku Zakia Lashku akishika nafasi ya pili.
Safari Field Challenge ni mashindano yanayofanyika kila mwaka kwa lengo la kuwatambua, kuwasherehekea na kuhamasisha ubora wa waongoza watalii nchini. Kupitia programu hiyo, washiriki na umma hupata fursa ya kujifunza, kutangaza vivutio vya utalii na kuburudika kupitia vipindi vinavyorushwa kwenye televisheni.







No comments:
Post a Comment