Monday, November 07, 2016

WAKUU WA MIKOA NA WILAYA WAASWA KUENDELEA KUTOA USHIRIKIANO KWA WAWEKEZAJI NCHINI

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru akiwasili katika kiwanda cha kutengeneza Vifungashio kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani kwa ajili ya kuweka Jiwe la Msingi, Katikati ni Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Mlingi Mkucha na kulia ni Mkurugenzi Muendeshaji wa Kiwanda hicho Bw. Joseph Wasonga. 
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru akisalimiana na baadhi ya wageni waliohudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Limited kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru akisaini kitabu cha wageni alipofika katika kiwanda cha kutengeneza Vifungashio kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani kwa ajili ya kuweka Jiwe la Msingi.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru (Katikati), Mkurugenzi Muendeshaji wa Kiwanda hicho Bw. Joseph Wasonga(kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Mlingi Mkucha wakielekea ndani ya kiwanda kuangalia mitambo na hatua iliyofikiwa kabla ya kuanza kazi ya kiwanda hicho.
Mitambo itakayotumika katika kuzalishia vifungashio ikiwa tayari imekwisha fungwa tayari kwa kuanza kazi.
Mkurugenzi Muendeshaji wa Kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Limited Bw. Joseph Wasonga na wafanyakazi wa kiwanda wakimtembeza Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru na kumpa maelekezo mbalimbali juu ya hatua iliyofikiwa kabla ya kiwanda hicho hakijaanza kufanya kazi na kuzalisha vifungashio
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Mlingi Mkucha akiongea wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Limited kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani na kuwataka watanzania wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya viwanda kupeleka maandiko ya miradi yao katika shirika hilo na watampa ushirikiano wa kutosha ili kuweza kutimiza lengo la serikali ya awamu ya tano ya kuwa na serikali ya viwanda.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bi. Asumpta Mshana akiongea wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Limited kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani na kumshukuru muwekezaji wa kiwanda hicho kwa kuamua kuwekeza katika mkoa wa pwani kwani itaisaidia kuongeza mapato katika mkoa na kuongeza ajira kwa wakazi.
Mkurugenzi Muendeshaji wa Kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Limited Bw. Joseph Wasonga akiongea wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda hicho na kuishukuru Serikali kupitia taasisi zake ikiwemo NDC, NEMC,TBS na Ofisi ya Mkoa wa Pwani kwa ushirkiano walioupata wakati wa mchakato wa uanzishaji wa Kiwanda hicho hadi hapo kilipofika na kuzitaka taasisi za fedha nchini kuendelea kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuwaaidia wawekezaji wazawa.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru akiongea wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Limited kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani ambapo alimpongeza muwekezaji wa kiwanda hicho na kutoa rai kwa wakuu wa wilaya na mikoa nchini kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya viwanda kama ilivyo katika mkoa wa Pwani.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru (katikati)akikata utepe kuashirika uwekaji wa jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani, wakwanza kushoto ni Mkurugenzi Muendeshaji wa Kiwanda hicho Bw. Joseph Wasonga, watatu kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Mlingi Mkucha akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bi. Asumpta Mshana. 
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru (katikati mwenye miwani), Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Mlingi Mkucha (mwenye tai nyekundu), Mkurugenzi Muendeshaji wa Kiwanda cha vifungashio Bw. Joseph Wasonga (wanne kutoka kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bi. Asumpta Mshana wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kiwanda hicho na wafanyakazi wa NDC.PICHA HABARI NA HASSAN SILAYO 


Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio kilichopo wilayani Kihaba mkoani Pwani Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru amesema kuwa tukiwa tunaelekea katika nchi ya viwanda serikali inajukumu la kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji nchini.Dkt. Adelhelm amesema kuwa viongozi hao hawana budi kuiga mfano wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wawekezaji ikiwemo kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika mkoa huo.

“Dhumuni la serikali kwa sasa ni kuhakikisha tunaifikia nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda,na hili tutalitekeleza pia kwa kushirikiana na sekta binafsi na ni jukumu la viongozi ikiwemo wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa nchini kote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji ikiwemo kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda”. Alisema Dkt. Adelhelm.

Dkt. Adelhelm aliongeza kuwa mpaka ifikapo mwaka 2020 Serikali imepanga kuhakikisha sekta ya viwanda nchini inachangia asilimia 15 kwenye pato la taifa kutoka asilimia 7.3 iliyopo hivi sasa.Pia Dkt. Adelhelm alisema kuwa Serikali imepanga kuongeza idadi ya ajira za viwandani na ajira zitokanazo na sekta ya viwanda hadi kufikia asilimia 40 ifikapo mwaka 2020.

Naye Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa(NDC) Bw. Mlingi Mkucha amesema kuwa shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza katika viwanda ikiwemo kupitia maandiko ya miradi yao na kuwasimamia ili kuhakikisha kwa pamoja wanatimiza lengo la serikali ya awamu ya tano ya kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.

Bw. Mkucha aliongeza kuwa katika wilaya ya Kibaha kuna hekari 330 zilizotengwa kwa ajili ya viwanda vya aina mbalimbali ikiwamo viwanda vya kuunganisha magari, vuwanda vya madawa na viwanda vya nguo hivyo kama kuna muwekezaji mwenye nia ya kuwekeza katika sekta hizo aende katika ofisi za Shirika hilo ili kuweza kujadili namna ya kutekeleza suala hilo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bi. Asumpta Mshana alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho katika mkoa wa pwani ni mwendelezo wa jitihada za kumuunga mkono Rais Magufuli ya kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Bw. Joseph Wasonga alishukuru jitihada za serikali na taasisi zake kwa ushirikiano wanaoupata tangu wakiwa na wazo la kuanzisha kiwanda hicho hadi kufikia hatua hiyo ya uzinduzi.

Bw. Wasonga aliongeza kuwa dhumuni la kiwanda hicho ni kuzalisha vifungashio milioni 16 hadi milioni 20 kwa mwaka na kuongeza zaidi idadi ya ajira kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka kiwanda hicho na maeneo ya jirani.Kiwanda cha hicho kinamilikiwa kwa ubia kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa(NDC) na kampuni ya Wande Printing and Packaging inayomilikiwa na mzawa.

No comments: