Tuesday, November 15, 2016

Makala-Tathmini ya Uchaguzi Mkuu 2015 yaonesha mafanikio

Mwenyekitiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) JajiMstaafu Damian Lubuva (kushoto) na Waziri wa Nchi Ofisi ya WaziriMkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na WalemavuMhe. JenistaMuhagama, wakioneshaVitabu vya Taarifa ya TathminiBaada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwanimwaka 2015, mjini Dodoma.
wenyekitiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) JajiMstaafu Damian Lubuva (kushoto) akimkabidhiWaziri wa Nchi Ofisi ya WaziriMkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na WalemavuMhe. JenistaMuhagama (kulia) Taarifa ya TathminiBaada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwaniwamwaka 2015, mjini Dodoma.
Waziriwa Nchi Ofisi ya WaziriMkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na WalemavuMhe. JenistaMuhagamaakihutubiamkutano wa kukabidhi Taarifa ya Tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwaniwamwaka 2015, mjini Dodoma.Kushoto niMwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) JajiMstaafu Damian Lubuvana kulia ni Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji Mst. wa Zanzibar Hamid Mahmoud Hamid.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani akitoamuhtasari wa matokeo ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015, mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) JajiMstaafu Damian Lubuva (kushoto) akitoamaenelezo ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015, mjini Dodoma.
Pichana Hussein Makame, NEC

……………………………………………………………………………..

Hussein Makame, NEC

Wahenga walisema “Safari bila ya dira huishia kupotea njia”. Baada ya kukamilika kwa Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Tume ya Taifa ya uchaguzi iliamua Kufanya tathmini ili kubaini utekelezaji wa uchaguzi mkuu.Katika utekelezaji wa mkakati wowote ni muhimu kuwa na dira ili kujua mafanikio au kushindwa kwa utekelezaji wa mkakati huo.

Baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilifanya tathmini ya Uchaguzi huo katika halmashauri 75 kwa kuwahoji na kujadiliana na wadau mbalimbali wa uchaguzi ili kupata mtazamo wao juu ya Uchaguzi huo.

Oktoba 28 mwaka huu, NEC imekabidhi Taarifa ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015 kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Muhagama kwa niaba ya Serikali, kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu Bungeni mjini Dodoma.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mst. Damian Lubuva anasema Tathmini hiyo imefanyika kuanzia tarehe 1 hadi 26 mwezi Februari, 2016 katika Mikoa 22 kati ya mikoa 30 iliyokuwepo wakati wa Uchaguzi huo, Halmashauri 64 kati ya 181, Kata 192 kati ya 3,953 za Tanzania Bara na Shehia 12 kati ya 386 za Tanzania Zanzibar.

Anabainisha kuwa lengo kuu la tathmini hiyo ni kupata mtazamo wa wadau juu ya taswira halisi ya Tume ili kujenga msingi bora wa kutekeleza chaguzi zijazo na kupata majibu ya changamoto zilizojitokeza kwenye Uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na kujua kwa nini baadhi ya maeneo yalikuwa na mwitikio mdogo wa kupiga kura ikilinganishwa na wapiga kura waliojiandikisha.

“Matokeo ya tathmini hii pia yataisaidia Tume katika kujitathmini katika maeneo ya kiutendaji ikiwamo kurekebisha Sheria, Kanuni, masuala ya kisera na kufanya mapitio ya Mpango Mkakati wa Tume na Mkataba wa Huduma kwa Mteja” anasema Jaji Mst. Lubuva.

Akizungumzia Tahmini hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani anasema takwimu za tathmini hiyo zimekusanywa kupitia mahojiano ya ana kwa ana kwa msaada wa madodoso na majadiliano ya makundi maalumu.

Anasema majadiliano yalijumuisha makundi maalum 192 ya wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 na makundi 192 ya vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 na kila kundi lilijumuisha kati ya watu 5 hadi 10 kwa kuzingatia jinsi pamoja na watu wenye ulemavu.

Bw. Kailima anabainisha kuwa sampuli ya watu waliohojiwa ilikuwa watu 1,915 ambapo kati yao 1,029 walikuwa Watendaji wa Uchaguzi, 499 wapiga kura na watumishi wa umma walikuwa 387 na kati yao wanaume walikuwa 1,184 sawa na asilimia 62 huku wanawake wakiwa 731 sawa na asilimia 38.

Kwa upande wa umri, Bw. Kailima anasema sampuli hiyo ilikuwa na vijana (miaka 18 – 35) 767 sawa na asilimia 40, umri kati ya miaka 36 – 60 walikuwa 1,085 sawa na asilimia 57 na umri zaidi ya miaka 60 walikuwa 63 sawa na asilimia 6.

Kwa mujibu wa Jaji Mst. Lubuva, wadau waliohojiwa ni pamoja na Watendaji wa Uchaguzi katika Ngazi mbalimbali wakiwemo Wasimamizi wa Uchaguzi, Makarani wa Uchaguzi, Makarani waongozaji, wasimamizi wa Vituo, Wasimamizi wasaidizi na Walinzi wa Vituo, Wapiga Kura, wananchi wa kawaida.

Bw. Kailima anasema kati ya wadau 1,915 waliohojiwa, wadau 727 sawa na asilimia 38 walitoka katika maeneo yaliyokuwa na mwitikio mkubwa, wahojiwa 238 sawa na asilimia 12 walitoka katika maeneo yaliyokuwa na mwitikio wa wastani na 950 sawa na asilimia 50 walitoka katika maeneo yaliyokuwa na mwitikio Mdog

Akitoa muhtasari wa matokeo ya tathmini hiyo kwa baadhi ya maeneo, Bw. Kailima anasemakuhusu Utaratibu wa Kupiga na Kuhesabu Kura, matokeo yanaonesha kuwa, jumla ya Watendaji na Wadau wa Uchaguzi 1,915 waliohojiwa, 1,895 sawa na asilimia 99 walibainisha kuwa taratibu zilifuatwa.

Kuhusu Kujumlisha Kura,jumla ya Watendaji wa Uchaguzi 1,029 walihojiwa, kati yao Watendaji 1,023 sawa na asilimia 99.4 walieleza kuwa, taratibu za Uchaguzi katika kujumlisha Matokeo zilifuatwa..” anasema Bw. Kailima

Kuhusu Taratibu za Kutangaza Matokeo, Bw. Kailima anasema matokeo yanaonesha kuwa, kati ya Watendaji 1,029 waliohojiwa, 1,003 sawa na asilimia 97.5 walisema taratibu zilizingatiwa katika kutangaza matokeo.

Kutokana na matokeo ya Tathmini hiyo, Jaji Mst. Lubuva anasema Tume imejiridhisha kupitia maoni ya wadau kwamba Sheria, Kanuni na maelekezo yaliyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu yalikuwa chachu ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu.

“Aidha, wadau wengi walionesha kuridhishwa na utendaji wa Tume katika kusimamia Uchaguzi Mkuu na kutangaza matokeo kwa kufuata Sheria na Kanuni zilizopo” anasema Jaji Mst. Lubuva.

Kuhusu mwitiko wa Wapiga Kura, Jaji Mst. Lubuva anasema kuwa Tathmini imeonesha kuwa katika baadhi ya maeneo watu waliojitokeza kupiga Kura ni wachache ikilinganishwa na idadi ya Wapiga Kura waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Akitaja sababu za hali hiyo, Jaji Mst. Lubuva anasema ni pamoja na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa kupiga kura kutokana na Elimu ya Mpiga Kura kutowafikia wapiga Kura wengi, Wapiga Kura walijiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kupata Kadi kwa ajili ya matumizi mengine na kuwepo hofu ya vitisho na vurugu siku ya kupiga Kura.

Ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye uchaguzi huo, Jaji Mst. Lubuva anasema wadau wamependekeza mambo mbalimbali ikiwemo Uboreshaji endelevu wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuitaka Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura kila mwaka.

“Wadau wamependekeza kuwa Serikali ifanye mapitio ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 na Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura 292 ili kurekebisha vifungu vinavyokinzana; na Serikali ibadili Muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuwa na Ofisi na Watumishi katika kila Halmashauri nchini na Ofisi Zanzibar” anasema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mhe. Jenista Muhagama anasema baada ya kupata maelezo ya matokeo ya tathmini, anashawishika kusema kuwa kwa kiasi kikubwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitekeleza majukumu yake ya Kikatiba kwa ufanisi mkubwa.

“Huu ni mfano na funzo kuwa Watanzania tukiamua kutimiza wajibu wetu kwa maslahi mapana ya Nchi hatutashindwa. Kinachotakiwa ni kuwa na dhamira ya dhati ya kufanikiwa kwa kila jambo tunalopanga kulitekeleza” anasema Waziri Mhagama.

Anaongeza kuwa kifungu cha 15 (5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura 343, Tume kinaagiza kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na mwingine, hata hivyo haikuwezekana kufanyika hivyo baina ya mwaka 2010 na mwaka 2015 kutokana na ufinyu wa Bajeti na kuchelewa kupatikana fedha kwa wakati.

“Kutokana na hali hiyo, naomba niseme kuwa Serikali itahakikisha kuwa, upungufu uliojitokeza unatatuliwa kwa kadri ya uwezo wetu ili kuiwezeshwa Tume kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba na Kisheria kwa ufanisi na kwa wakati”

Akizungumzia Elimu ya Mpiga Kura, Bw. Kailima anasema Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina wajibu wa Kisheria na Kikanuni wa kutoa Elimu ya Mpiga Kura, Kuratibu na Kusimamia watu na Taasisi zinazotaka kutoa Elimu hiyo.

Anasema uzoefu unaonesha elimu ya Mpiga Kura hutolewa wakati wa Uchaguzi Mkuu na hasa kipindi baada ya Uteuzi wa Wagombea na hukoma mwisho wa Kampeni za Uchaguzi huku Taasisi na Asasi zinazotoa elimu hiyo nazo zikiomba kibali cha kutoa elimu hiyo kipindi cha uchaguzi tu.

Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi anasema ili kutekeleza matakwa ya Sheria, Tume itatoa Elimu ya Mpiga Kura kwenye maonesho mbalimbali, Mikutano inayojumuisha wadau wa Uchaguzi na kwenye Shule za Sekondari na vyuo vikuu nchini.

Anasema hadi sasa Tume imeshatoa Elimu hiyo kwenye maonesho ya Sabasaba, Nanenane, Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania, Wiki ya Vijana Kitaifa, na kutembelea Shule za Sekondari za Wilaya za Kondoa (Dodoma), Uvinza (Kigoma), Ubungo (Dar es salaam), Manispaa ya Musoma (Mara), na Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Mbali na njia hizo, anaongeza kuwa Tume itatoa Elimu hiyo kwa kuhudhuria na kutoka Elimu hiyo katika Mikutano ya Viongozi wa Dini, Kamati za Ushauri za Mikoa na Wilaya, Mabaraza ya Madiwani na Mikutano Mikuu ya Vijiji na Mitaa.

“Aidha Tume itahudhuria na kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika vikao au mikutano itakayowajumuisha viongozi mbalimbali kama Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya na Jeshi la Polisi” anasema Bw. Kailima na kuongeza kuwa:

“Tume pia itaanzisha klabu za Uchaguzi katika shule za Sekondari angalau moja kwa kila Mkoa kwa kuanzia. Lengo likiwa ifikapo mwaka 2019, kila Wilaya katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iwe na Klabu ya uchaguzi katika shule moja ya Sekondari”

“Tume itatembelea vyombo vya habari na kukutana na watumishi wake, na vipindi mbalimbali vya Luninga na Radio na kuzichapisha makala katika magazeti na mitandao ya Kijamii na kutoa vibali vya kutoa elimu ya Mpiga Kura kwa Taasisi na Asasi”

Bw. Kailima anaamini kuwa Elimu ya Mpiga Kura ikitolewa katika kipindi chote cha mwaka itawezesha wananchi na wadau kupata taarifa sahihi kuhusu Tume, Kazi, Wajibu na Majukumu yake, kufahamu utaratibu wa Uandikishaji wa Wapiga Kura.

Anasema kupitia Elimu hiyo, wananchi na wadau watafahamu taratibu na hatua zote za Uchaguzi hadi kutangaza matokeo na kujua umuhimu na thamani ya wao kushiriki katika shughuli za mchakato mzima wa Uchaguzi na kuzingatia taratibu zote.
Post a Comment