Wednesday, November 09, 2016

MWILI WA MAREHEMU SPITA MSTAAFU SAMUEL SITTA KUWASILI KESHO ALASIRI JIJINI DAR


Mwili wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mstaafu wa  Mhe. Samuel Sitta unatarajiwa kuwasili kesho Alhamisi Novemba 10, 2016 majira ya saa 9:00 alasiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Mwili huo unatarajiwa kupokelewa na Viongozi Mbalimbali wa Kitaifa wa Chama na Serikali katika eneo la Terminal I.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa leo Jijini Dar es Salaam na Ofisi ya Waziri Mkuu, mara baada ya kupokelewa katika uwanja wa ndege, mwili huo utapelekwa nyumbani kwake Masaki jijini Dar es saam.

Aidha, taratibu za viongozi mbalimbali na wanaombolezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Mhe.Sitta zitafanyika katika Viwanja vya Karimjee siku ya Ijumaa ya tarehe 11 Novemba ,2016 kuanzia majira ya saa 1:30 asubuhi.

Mara baada ya zoezi hilo kukamilika mwili wa Marehemu Sitta utapelekwa uwanja wa ndegewa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea mkoani Dodoma siku ya Ijumaa tarehe 11 Novemba, 2016.

Mwili huo utawasili mkoani Dodoma majira ya saa 8 mchana na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma na Bunge.

Baadae mwili huo utapelekwa katika Viwanja vya Bunge ambapo salamu mbalimbali zitatolewa na Spika, Waziri Mkuu , Kambi Rasmi ya Upinzani na viongozi wa Mkoa wa Dodoma.

Mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Waheshimiwa Wabunge na waombelezaji mbalimbali walioko katika Viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma watatoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu na baadaye kupelekwa Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Urambo mkoani Tabora kwa ajili ya mazishi.

Mwili wa Marehemu Sitta unatarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Tabora majira ya saa 10 jioni ya 11 Novemba, 2016 na baadae kusafirishwa kuelekea nyumbani kwake Wilayani Urambo ambapo utawasili majira ya saa 12 jioni.

Viongozi na waombezaji mbalimbali Wilayani Urambo mkoani Tabora watatoa heshima za mwisho siku ya Jumamosi tarehe 12 Novemba, 2016 kuanzia asubuhi na mazishi yanatarajia kufanyika siku hiyo hiyo majira saa 9 alasiri.

Marehemu Mhe. Sitta alizaliwa 18 Desemba, 1942 Urambo Mkoani Tabora

Imetolewa na Idara ya Habari- Maelezo
9 Novemba, 2016
Post a Comment