Na Jacquiline Mrisho na Eleuteri Mangi – MAELEZO, Dodoma.
Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umepitisha rasmi Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 ambapo hatua inayofuata ni kuridhiwa na kusainiwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili uwe Sheria kamili ya nchi.
Muswada huo umepitishwa jana Bungeni mjini Dodoma ambapo mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mhe. Andrew Chenge.Wabunge walijadili Muswada huo kifungu kwa kifungu na kuunga mkono upitishwaji wake baada ya Waziri mwenye dhamana na habari kutoa hoja ili Muswada huo uweze kujadiliwa.
Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kupitishwa Muswada huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye amewashukuru wadau wote walioshiriki katika kutoa maoni juu ya Muswada huo kwani ndiyo yamepelekea kukamilisha mchakato mzima wa Muswada huo.
“Kwa niaba ya Serikali napenda kuwashukuru wadau wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kuhakikisha tunatimiza malengo ya takribani miaka 20 iliyopita ya kuifanya taaluma hii ya habari kuheshimika kama zilivyo taaluma zingine”, alisema Waziri Nape.
Waziri Nape ameongeza kuwa kwa sasa Muswada huo umeshapitishwa hivyo kilichobaki ni utungaji wa Kanuni ambapo ameomba wadau wa tasnia ya habari kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa maoni yatakayopelekea kuwa na kanuni zenye tija kwa wanahabari na taifa kwa ujumla.
Aidha, Mhe. Nape amewaasa wadau wa habari kuunganisha nguvu kwa pamoja hasa katika kipindi hiki ambacho Muswada huo umepitishwa pia amewataka wadau hao wasiruhusu mgawanyiko utokee kati yao bali washirikiane na Serikali katika kutekeleza wajibu wao wa kihabari kwa jamii.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju amesema kuwa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 ni mwanzo mpya wa tasnia ya habari nchini ambapo amewaasa wadau wa habari wakiwemo waandishi wa habari kutambua kuwa haki mara zote huendana na wajibu, hivyo hakuna haki isiyo na wajibu.
Muswada huo uliopitishwa jana umejadiliwa na Bunge hilo kwa siku mbili ambapo kwa mara ya pili ulisomwa mbele ya Kamati ya Bunge zima na hatimaye kusomwa kwa mara ya tatu ili kukidhi hatua za utungwaji wa Sheria nchini.
Comments