SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UUZWAJI WA NYUMBA ZA MRADI WA UJENZI WA MINDU, DAR ES
SALAAM
Kwa mara nyingine tena Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) leo 24 Oktoba, 2012 limezindua rasmi mauzo ya nyumba katika mradi
wake mpya wa Mindu, jijini Dar es Salaam. Ujenzi wa mradi huu ulianza rasmi mwezi
Novemba mwaka 2011, na unatarajiwa
kukamilika rasmi Aprili 2013 na mteja kuweza kukabidhiwa nyumba yake mwezi
Mei 2013, ikiwa ni miezi 18 baada ya
kuanza ujenzi.
Mradi unatarajiwa kugharimu kiasi cha
zaidi ya Shilingi bilioni 11 mpaka utakapomalizika, fedha zinazogharamiwa na
Shirika kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo fedha za mikopo ya benki.
Mradi huu uliopo mtaa wa Mindu eneo la Upanga, takribani mita
100 kutoka Hospitali Kuu ya Taifa Muhimbili, una sehemu ya nyumba 60 za kuuzwa
zilizopo kwenye majengo pacha ya ghorofa 15, uko sehemu zenye huduma zote
muhimu za kijamii zikiwamo hospitali,
shule, maduka, na masoko.
Pia Mradi unatarajiwa kuboresha maisha ya
wanunuzi wa nyumba hizi kwani upo karibu kabisa na katikati ya jiji na kwamba
mnunuzi anaweza kwenda kazini bila kutumia gharama yoyote ya usafiri wa
gari. Aidha, nyumba zipo ndani ya uzio
kwa ajili ya usalama wa wakaazi wake na
kuna maegesho ya magari ya kutosha.
Nyumba 60 tu zinazouzwa ambapo kila nyumba ina vyumba vitatu
vya kulala, vyo vinajitegemea. Kila nyumba ina ukubwa wa mita za mraba 141 (sq.m),
sebule iliyoungana na eneo la kula chakula, choo cha umma, jiko kubwa la kisasa
na eneo la kufulia na kuanikia nguo.
Sifa za ziada za mradi huu ni kuwa na eneo
maalum la kukusanyia taka, sehemu iliyotengwa maalum kwa ajili ya kufanyia
mazoezi (gym), bwawa la kuogelea (swimming pool) na eneo kubwa la ziada la
maegesho ya magari.
Kila nyumba itauzwa kwa bei ya TZS
272,050,673.08 bila kodi ya ongezeko la thamani (VAT ) na TZS
321,019,794.24 ikiwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Tunawahamasisha na kuwakaribisha watanzania wote walio
nchini na nje ya nchi kujitokeza ili kununua nyumba hizo. Wanaweza kufanya
mawasiliano na Makao Makuu ya Shirika, Ofisi zetu za Mikoa au kupitia barua
pepe na kukamilisha taratibu mapema kwa ajili ya kuweza kuingia kwenye mchakato
ulio wazi wa manunuzi.
Katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa
nyumba, Shirika linajenga nyumba za gharama ya juu, kati na chini ili
kuwahudumia watanzania wa kada zote. Katika azma hiyo, nyumba 10,000
zitakazojengwa kufikia 2015 zitahusu watu wa
kipato cha juu na nyumba 5,000 zitakazojengwa kufikia mwaka huo zitakuwa
ni nyumba za watu wa kipato cha chini.
Shirika limeanza kujenga nyumba za gharama ya
kati na juu ili kupata faida itakayoliwezesha kuwajengea watu wa kipato cha
chini nyumba za gharama nafuu. Hii inatokana na ukweli kuwa Shirika halipati
ruzuku toka serikalini ya kujenga nyumba kwa ajili ya wananchi wa kipato cha
chini. Mradi huu wa Mindu tunaouzindua hii leo, ni moja ya miradi ya ujenzi wa
nyumba za watu wenye kipato cha juu..
Ukiwa mdau na mnunuzi
mtarajiwa, ama una ndugu/rafiki anayetamani kununua nyumba katika mradi huu, tafadhali
waweza kutumia akaunti nambari : …….. au wasiliana na Kitengo cha Mauzo simu namba 0754 444 333; barua pepe:
sales@nhctz.com na pia tembelea tovuti ya Shirika www.nhctz.com kwa maelezo zaidi.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO NA HUDUMA KWA JAMII
SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA
2 comments:
Yaani nyumba Dar bei ghali kuliko Marekani? Whaaaaaaat????
Siyo elimu tu kaka bali hata Afya kwa maana ya matibabu, elimu ya aina yoyote ile, maana kindergaten siku hizi ni kama chuo kikuu, usafiri ukipanda ndege kutoka dar kwenda mwanza nighali kuliko hata toka new york pengine kwenda hata washington kwa maana ya internal flight. Namba yangu nimekurushia kaka yako kila nikipiga sikupati sijui kuna sehemu nakosea najaribu tena hiyo hapo 0784746157
Post a Comment