Tuesday, March 10, 2026

BILIONEA ROSTAM AZIZI AANDIKA HISTORIA: ACHUKUA UMILIKI MKUBWA WA NATION MEDIA GROUP, AFUNGUA ENZI MPYA YA UWEKEZAJI WA KIMKAKATI AFRIKA MASHARIKI


Mfanyabiashara maarufu nchini TANZANIA, Rostam Aziz, ameandika historia mpya katika sekta ya habari baada ya kukamilisha ununuzi wa hisa asilimia 54.08 za kampuni ya kimataifa ya vyombo vya habari, Nation Media Group (NMG).

Kwa maana hiyo Mmfanyabiashara huyo ameinunua kampuni ya vyombo vya habari ya Kenya ya Nation Media Group yenye makao makuu yake jijini Nairobi nchini Kenya. 

Kupitia moja ya kampuni zake, Aziz amenunua asilimia 100 ya NPRT Holdings Africa Limited – chombo cha uwekezaji kilichokuwa kinamiliki hisa 92,618,177 za kawaida katika NMG kwa niaba ya Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED). Hatua hiyo inamfanya kuwa mbia mkuu wa taasisi hiyo kubwa ya habari Ukanda wa Afrika Mashariki.

Mauzo hayo yanaashiria kufungwa kwa ukurasa wa kihistoria wa ushirikiano wa miaka 66 kati ya NMG na AKFED, uliodumu tangu mwaka 1959, wakati Prince Karim Aga Khan IV alipoanzisha East African Newspapers (Nation Series) Ltd na kununua gazeti la Kiswahili la Taifa Leo. 

Tangu hapo, NMG imekua na kuwa kongamano kubwa la vyombo vya habari vinavyomiliki zaidi ya chapa 30 katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku takwimu za hivi karibuni zikionyesha kufikia zaidi ya watumiaji milioni 62 wa majukwaa ya kidijitali.

Ingawa thamani halisi ya muamala huo haijawekwa wazi, wachambuzi wa sekta ya habari wanautazama kama moja ya miamala mikubwa zaidi katika tasnia ya habari Afrika Mashariki katika miongo ya karibuni.

Kwa Azizi, uwekezaji huu ni kama kurejea nyumbani katika sekta ya mawasiliano. Hapo awali aliwahi kushiriki kuanzisha kampuni ya mawasiliano iliyozindua machapisho yenye ushawishi mkubwa nchini Tanzania, ambayo baadaye yalinunuliwa na NMG.

Miongoni mwa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Nation Media Group ni Gazeti la Daily Nation, The East African, Daily Monitor, Taifa Leo, Business Daily, Television ya NTV.

Lakini pia inamiliki vyombo vya habari vilivyopo TANZANIA na Uganda ikiwemo Magazeti ya The Citizen, Mwananchi na mwanaspoti Tanzania.

Akizungumza kufuatia ununuzi huo, Aziz amesisitiza dhamira yake ya kulinda uhuru wa uhariri wa NMG huku akiwekeza zaidi katika mageuzi ya kidijitali na upanuzi wa wigo wa kampuni hiyo katika soko la kikanda.

“NMG ni taasisi yenye umuhimu mkubwa kwa Afrika Mashariki. Tutaendelea kulinda uhuru wake wa uhariri na kuwekeza katika mafanikio yake ya baadaye kama shirika huru na kinara wa habari katika ukanda huu,” ameeleza Azizi.

Kwa sasa, muamala huo unasubiri kukamilika kwa taratibu za kisheria na idhini za mamlaka husika, hatua inayotarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu hadi minne ijayo.

Hatua hii inaashiria kuimarika kwa uwekezaji wa Watanzania katika taasisi za kimkakati za kikanda, huku ikiibua matarajio mapya ya ubunifu, ukuaji wa kidijitali na ushindani chanya katika tasnia ya habari Afrika Mashariki.



No comments:

BILIONEA ROSTAM AZIZI AANDIKA HISTORIA: ACHUKUA UMILIKI MKUBWA WA NATION MEDIA GROUP, AFUNGUA ENZI MPYA YA UWEKEZAJI WA KIMKAKATI AFRIKA MASHARIKI

Mfanyabiashara maarufu nchini TANZANIA , Rostam Aziz , ameandika historia mpya katika sekta ya habari baada ya kukamilisha ununuzi wa hisa a...