Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Bi. Gloria Komba, amepokea rasmi mkataba wa ujenzi wa jengo la kuchakata mafuta ya alizeti lililopo katika Kijiji cha Nyangulu, kutoka kwa Mratibu wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayanuai Tanzania (SLR), Dkt. Damas Mapunda.
Mradi wa SLR, unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, unalenga kurejesha mazingira yaliyoharibika, kuboresha mifumo ya ikolojia, na kuendeleza maisha bora ya jamii zinazozunguka maeneo yanayotekelezwa miradi hii. Kiwanda hiki cha kuchakata mafuta ya alizeti kitakuwa ni kipengele muhimu cha kuimarisha kilimo cha alizeti na kuongeza kipato kwa wakulima wadogo wa kijiji cha Nyangulu na maeneo jirani.
Makabidhiano ya mkataba yamefanyika leo, Agosti 22, 2025, wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Ofisi ya Makamu wa Rais, waliotembelea wilaya ya Mbarali ili kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Mradi wa SLR. Ziara hii imekuwa fursa ya kuthibitisha jinsi miradi ya kiasili na ya maendeleo ya kijamii inavyotekelezwa, ikiwapa wadau na viongozi fursa ya kuona matokeo ya uwekezaji na juhudi za kurejesha mazingira na kuimarisha ustawi wa jamii.
Mradi wa SLR unadhihirisha azma ya serikali ya kuendeleza miradi endelevu ya mazingira, huku ukiwa ni mfano wa ushirikiano kati ya serikali, jamii na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha maendeleo ya kiikolojia na kijamii yanapatikana kwa usawa.
No comments:
Post a Comment