Thursday, October 27, 2016

WAZIRI LUKUVI ATOA TAARIFA KUHUSU UTAPELI UNAOFANYWA KWA KUTUMIA NYARAKA ZA KUGHUSHI ZA BARUA ZINAZODAIWA KUTOLEWA NA HALMASHAURI YA JIJI LA DAR ES SALAAM

Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe. William Lukuvi akionesha nyaraka zilizoghushiwa na mmoja wa raia wa kigeni Bw. Hamant Patel alizotumia kujipatia fursa ya kumiliki ardhi kama raia. 
Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe. William Lukuvi akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake. 
…………………………………………………… 

Katika siku za hivi karibuni kumetokea wimbi kubwa la matapeli wanaotumia nyaraka za kughushi zinazodaiwa kuwa ni Barua za Toleo zilizotolewa na iliyokuwa ofisi ya ardhi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam. Nyaraka hizo za kughushi zimesababisha wananchi kupoteza fedha na mali na kuongezeka kwa migogoro mingi ya ardhi katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dare es salaam. 

Napenda kuwatahadharisha watendaji na umma wote kwa ujumla kuwa waangalifu wakati wa kuingia kwenye miamala ya mauziano au utayarishaji wa hati milki kwa kutumia nyaraka za aina hiyo. Hivyo kuanzia sasa kusifanyike muamala wala utayarishaji wa hati yoyote kwa kutumia nyaraka za aina hiyo mpaka ziwe zimehakikikwa na Kamishna wa Ardhi. Aidha, kwa wananchi wanaojihusisha na utumiaji au utayarishaji wa nyaraka za kughushi watambue kuwa hilo ni kosa kisheria na watakaobainika Wizara itahakikisha sheria inachukua mkondo wake. 

Ninaagiza wananchi wote wenye nyaraka halali zilizotolewa na iliyokuwa Ofisi ya Ardhi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam, wazirejesha kwa ofisi ya Kamishna wa Ardhi. Ofisi hiyo itaweka mpango maalumu wa kuhakiki na kutoa Hati Milki. Atakaye leta nyaraka za kughushi atakamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya dola. 

B: UVAMIZI WA MAENEO YA UMMA, MASHAMBA NA VIWANJA VYENYE HATI MILKI 

Nimepokea taarifa za kuwepo kwa uvamizi mkubwa wa mashamba na viwanja vinavyomilikiwa kisheria. Uvamizi huo unafanywa kwa vizingizio mbalimnbali ikiwemo wavamizi kudai kuwa ni mapori, uhaba wa ardhi na sababu nyinginezo zisizo za kisheria. Kuvamia shamba au kiwanja ni kosa la jinai kwa mujibu wa fungu la 175 la Sheria ya Ardhi Na. 4 (1999). 

Ninazo taarifa pia za uvamizi mkubwa katika maeneo ya Mabwepande, Pugu Kajiungeni na maeneo ya Bagamoyo na maeneo mengine nchini. Ninazo taarifa pia baadhi ya viongozi wanashiriki katika kusaidia uvamizi wa viwanja na mashamba ya watu. Na wavamizi hawa wamethubutu hata kuwatisha maofisa wetu wanapokuwa kazini. Tabia hii haiwezi kuvumiliwa na lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe. Sheria inaweka wajibu wa msingi kwa vyombo vya dola, Halmashauri na wamiliki kulinda haki za kumiliki ardhi. 

Ninamwagiza Kamishna wa Ardhi, na Makamishna Wasaidiziwa Kanda kuweka mkakati maalum wa kukomesha tabia hiyo ya uvamizi kwa kushirikiana na vyombo vya dola na ofisi za Halmashauri. 

C: UDANGANYIFU WA URAIA KWA AJILI YA KUJIPATIA MILIKI ZA ARDHI 

Sheria za ardhi zinaelekeza kuwa ardhi ya Tanzania itamilikishwa kwa raia wa Tanzania. Wageni wanayo fursa ya kupata ardhi hiyo ikiwa wataihitaji kwa ajili ya uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC). 
Tunazotaarifa kuwa baadhi ya wageni (foreigners) wakishirikiana na raia hufanya udanganyifu na kughushi nyaraka za uraia ili kujipatia miliki za ardhi kama raia. Udanganyifu huo umekuwa pia ukifanywa na makampuni ambayo hujisajili kama makampuni raia kwa kutoa hisa nyingi kwa raia na mara baada ya kupata ardhi huhamisha hisa zote kwenda kwa wageni. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 (1999) Kampuni ni raia iwapo tu hisa nyingi (majority shares) katika kampuni hiyo zinamilikiwa na raia. Inapotokea mabadiliko ya umiliki wa hisa kwenye kampuni kupelekea hisa nyingi kumilikiwa na wageni, Kampuni hiyo inakoma kuwa raia kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 (1999) na inakosa sifa ya kumiliki ardhi kama raia tangu siku ambayo itasomeka hisa nyingi zinamilikiwa na wageni. 

Tumeanza sasa kazi ya kuhakiki kwa kushirikiana na Msajili ya Makampuni (BRELA) makampuni yote yanayomiliki ardhi kama raia ili kubaini kama bado yana sifa ya kumili ardhi kama raia. Na iwapo itabainika kuwa kampuni imepoteza sifa ya uraia, hatua za kisheria zitachukuliwa juu ya miliki ya ardhi inayomilikiwa na Kampuni hiyo ikiwemo kurejesha ardhi hiyo mikononi mwa serikali. 

Kwa wageni ambao wameghushi nyaraka za uraia na kujipatia fursa ya kumiliki ardhi kama raia, tumeweka mkakati maalum kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji kuwabaini na mara ikithibitika tutafuta miliki zao. 

Nawatakia Siku Njema 

William Vangimembe Lukuvi (Mb) 

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI

Post a Comment