Friday, October 28, 2016

WAZIRI PROFESA MBARAWA AZINDUA BODI YA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA JIJINI DAR ES SALAAM


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania, Dk. Haruni Kondo.
Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Fortunatus Kapinga, akizungumza kuhusu shirika hilo, kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Haruni Kondo, kuzungumza wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya shirika hilo jijini Dar es Salaam leo.(Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta, Fortunatus Kapinga, akizungumza kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya shirika, Dk. Haruni Kondo.
Mameneja wa Shirika la Posta Tanzania, wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa bodi mpya ya shirika hilo.
Baadhi ya wajumbe wa bodi mpya ya Shirika hilo, wakiwa katika uzinduzi wa bodi hiyo.
Baadhi ya wajumbe wa bodi mpya wakiwa katika uzinduzi wa bodi hiyo.
Meneja Mkazi Zanzibar wa shirika la Posta, Mwanaisha Saidi (katikati), Meneja wa Huduma za Barua, Fadya Zam (kulia) na Meneja Utumishi wa shirika, William Makumba (kushoto), wakiwa katika uzinduzi wa bodi hiyo.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia matukio mbalimbali katika uzinduzi wa bodi hiyo.
Baadhi ya viongozi wa Shirika la Posta wakiwa katika uzinduzi wa Bodi mpya ya Shirika hilo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania, Dk. Haruni Kondo, akitoa maelezo mafupi kuhusu bodi hiyo mpya pamoja na shirika hilo kwa jumla kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), kabla waziri Mbarawa hajaizindua rasmi bodi hiyo. Kushoto Ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo (Mawasiliano), Profesa Faustine Kamuzora.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Mawasiliano), Profesa Faustine Kamuzora, akitoa hutuba yake kabla ya kumkaribisha Waziri wa wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa (katikati), kutoa hotuba yake ya uzinduzi wa Bodi mpya ya Shirika la Posta Tanzania leo, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi wa Shirika la Posta wakinukuu hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Profesa Makame Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Profesa Makame Mbarawa, akizungumza wakati alipoizindua rasmi bodi mpya ya Shirika la Posta Tanzania, leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk. Haruni Kondo.
Baadhi ya wajumbe wa bodi ya Shirika la Posta wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Profesa Makame Mbarawa, alipokuwa akitoa hotuba yake ya uzinduzi wa bodi hiyo, leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Profesa Makame Mbarawa, akizungumza wakati akiizindua rasmi bodi mpya ya Shirika la Posta Tanzania, leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk. Haruni Kondo.
Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta, Fortunatus Kapinga (kushoto), akifuatilia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya shirika hilo, leo jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Bodi, Stella Nghambi, akitoa neno la shukurani baada ya Waziri Profesa Mbarawa kuizindua bodi hiyo.
Picha ya Pamoja ya Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati waliokaa), mara baada ya kuizindua bodi hiyo leo jijini Dar es Salaam.  
Picha ya Pamoja ya viongozi wa Shirika la Posta na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto waliokaa), mara baada ya kuizindua bodi hiyo leo jijini Dar es Salaam.  


HOTUBA YA MHESHIMIWA PROFESA MAKAME MBARAWA (MB) WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO WAKATI WA UZINDUZI WA BODI MPYA YA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA,TAREHE 20 OKTOBA, 2016, KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO, GHOROFA YA 12, POSTA HOUSE MAKAO MAKUU.

·         Katibu Mkuu wa Mawasiliano,
·         Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania,
·         Wakurugenzi wa Bodi, 
·         Kaimu Postamasta Mkuu,
·         Viongozi wa Menejimenti,
·         Wageni waalikwa,
·         Mabibi na Mabwana,

·            PONGEZI NA SHUKRANI
          
Awali ya yote napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uhai na afya  njema ya kuweza kujumuika hapa leo na kushiriki katika uzinduzi huu wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania.

Pia nawapongeza Wajumbe wote wa Bodi na Mwenyekiti kwa kuteuliwa kuongoza Shirika hili.

Ninawashukuru kwa kunikaribisha ili niungane na kuzungumza nanyi wakati huu wa kuzindua Bodi mpya.  Fursa hii ni adimu kwani imetuwezesha kufahamiana pamoja na kutafakari kwa kina juu ya changamoto zilizopo na kuanza kubuni njia ya kuzitatua.

·            MAJUKUMU NA CHANGAMOTO ZA SHIRIKA

                   Mwenyekiti wa Bodi,

Leo hii nitawakabidhi baadhi ya nyenzo na nyaraka za majukumu ya Shirika na Bodi ya Wakurugenzi kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Bunge Na. 19 ya mwaka 1993.

Sina haja ya kutaja majukumu haya lakini ni vyema kuanzia sasa mzingatie kuwa mawasiliano haya kwa njia ya Posta ni kichocheo  na kielelezo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Taifa lolote duniani.

Kwa bahati nzuri Wajumbe wa Bodi hii ni wataalamu wenye uzoefu na waliobobea katika nyanja muhimu ikiwa ni pamoja na uhamasishaji wa biashara, usimamizi wa rasilimali watu na rasiliamali fedha, sheria, TEHAMA, ubunifu katika biashara, usalama na uendeshaji wa sekta binafsi.

·            HALI YA HUDUMA ZA POSTA KITAIFA NA KIMATAIFA

Mwenyekiti wa Bodi,

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Posta Duniani (UPU), mtandao wa mawasiliano kwa njia ya Posta unajumuisha Ofisi za Posta laki sita na sitini elfu (660,000).

Huu ni mtandao mkubwa zaidi duniani ambao pamoja na huduma nyingine una uwezo wa kusambaza wastani wa barua zipatazo 450 bilioni na vifurushi 6 bilioni kwa mwaka.

Hapa Tanzania Shirika hili linaendesha mtandao wa Ofisi za Posta zipatazo 400. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo wastani watu 120,000 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanahudumiwa na ofisi moja ya Posta.  Kuhusu ufikishaji barua na vifurushi katika ofisi na makazi  ya watu (physical delivery of mail) kiwango ni kidogo sana.  Wastani wa 98% ya barua zinazohudumiwa na Shirika hili hupitia katika masanduku ya barua yalioko katika ofisi za Posta.

Kiwango hicho kinaonyesha wazi kuwa tunalo jukumu la msingi la kupanua na kuboresha mtandao wa huduma za Posta hapa nchini ili kufikisha huduma za kisasa za kimtandao karibu na jamii.  Ningependa kusisitiza hapa kuwa ni lazima Shirika hili liongeze kasi zaidi katika kuboresha na kuanzisha huduma zinazozingatia matakwa ya wateja.

·              SERA YA TAIFA YA POSTA
          Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi,

Kwa hivi sasa Wizara yangu inaendelea kuhuisha Sera ya Taifa ya Posta ili kuzingatia mahitaji ya sasa na baadae. Utekelezaji wa sera hii ni eneo mojawapo ambalo inabidi tulizingatie.

Mwelekeo wa sera hii kwa muhtasari ni:-

·         Kuwezesha Shirika la Posta ambalo ni mtoa huduma kwa umma (Public Operator) kutoa na kufikisha huduma bora kwa jamii yote na kwa gharama nafuu.

·         Kuliendesha Shirika la Posta kwa misingi ya kibiashara.

·         Kuzifanya huduma za Posta kuwa za kisasa zaidi kwa kutumia teknolojia maridhawa ili kukidhi mahitaji mapya ya wateja ambayo  yanabadilika mara kwa mara.

·         Kushirikisha sekta binafsi katika kuendesha na kuwezesha shughuli za Posta ili kuchochea maendeleo ya sekta hiyo na sekta nyingine kama za fedha, biashara,  afya, elimu, habari n.k

·         Wizara yangu inapenda kuona utekelezaji wa masuala yaliyoainishwa katika sera ya Posta na kuhakikisha uhuishwaji wa sera hii ambayo ni ya muda mrefu 2003 ili kuwezesha malengo yanafikiwa.

·            MATUMIZI SAHIHI YA FURSA NA RASILIMALI ZA SHIRIKA

Kwa bahati nzuri Shirika la Posta ni moja ya Taasisi zenye rasilimali na fursa nyingi ambazo kama zikitumiwa vizuri zinaweza kusaidia kuliendeleza Shirika.  Rasilimali na fursa hizo ni pamoja  na:-

·         Viwanja na majengo ya kuishi na ya ofisi ambayo yako sehemu mbalimbali hapa nchini na hasa yaliyopo maeneo ya mijini.  Kwa mfano, Shirika lina viwanja 178 na kati ya hivyo viwanja 153 vimeendelezwa na 25 havijaendelezwa.

·         Mtandao mpana wa ofisi za Posta zipatazo 400 hapa nchini ambao umeunganishwa katika ofisi za Posta zipatazo 660,000 duniani kote (Global Connectivity).

·         Uwezo mkubwa wa kutoa huduma unganishi za kimtandao (Integration of physical and digital solutions).

·         Uwezo mkubwa wa kuboresha huduma na biashara zilizopo na hapo hapo kuanzisha mpya .  Kwa bahati nzuri hata Sheria iliyoanzisha Shirika hili  inasisitiza juu ya jambo hili.

·         Mna uwezo wa kurejesha imani kubwa ya kihistoria (Historical Loyalty) waliyonayo wateja na wadau mbalimbali wa Posta.

Naamini mnafahamu kuwa  mkakati huu wa kutumia vizuri fursa na rasilimali kama hizi umefanywa na mashirika mengi ya Posta hapa duniani na umeyawezesha mashirika hayo kuwa na mafanikio makubwa.  Hali ni hivyo hivyo hapa nchini kwani, baadhi ya mashirikia kama hili la Posta yametumia vizuri fursa na rasilimali zilizopo na kuweza kufanikiwa.

Jambo la msingi  ni kuangalia maeneo yote hasa sheria zenye ukiritimba zinazozuia Shirika kutumia rasilimali zake kwa ajili ya uzalishaji mfano, sheria ya Shirika kuwa chini ya uangalizi wa Consolidated Holding Corporation (CHC)  ambapo haliwezi kukopa au kuweka rehani vitega uchumi vyake ili kuendeleza huduma na biashara.

·            MFUMO WA ANUANI ZA MAKAZI NA SIMBO ZA POSTA

Mwenyekiti na Wajumbe,

Anuani za makazi na simbo za posta (Physical Address and Post code System) ni moja ya mradi mkubwa wa kitaifa ambao mwezi Septemba mwaka huu Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa alizindua muongozo wake mkoani Dodoma.

Aidha, kuwepo kwa anuani zinazotambulisha makazi ya watu na rasimali za kudumu kutatoa fursa nyingi zaidi katika utoaji na uendeshaji wa huduma za posta nchini.

Ingawa wadau wa utekelezaji wa mfumo huu ni wengi lakini Wizara yangu na taasisi zilizoko chini yake hususani Shirika hili la Posta, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) zina wajibu mkubwa zaidi katika kuhakikisha manufaa ya mfumo huu yanawafikia watumiaji wa mwisho ambao ni pamoja na wananchi wa kawaida (last mile Users).  Manufaa hayo ni pamoja na:-

·         Kuwezesha huduma za usambazaji na logistiks.  Hili ni eneo linalopanuka kwa haraka sana hapa nchini na duniani kote.

·         Kuwezesha huduma jumuishi za kimtandao hususani za biashara (E-business), elimu (E-education), afya (E–medicine), utawala  serikalini (E – governance) na nyinginezo.

·         Uboreshaji wa huduma za dharura na usalama kama zima moto na uokoaji, polisi, magari ya wagonjwa, majanga kama matetemeko, mafuriko na vimbunga.

·         Kurahisisha usajili wa huduma, biashara, na mifumo mbalimbali kama vizazi, vifo, ndoa na talaka.

·         Kukuza utalii wa ndani na nje pamoja na kurahisisha utambuzi wa sehemu kwa wageni.

·         Kuboresha utendaji wa taasisi nyingine kama za Ugavi wa Nishati na Maji, Mabenki, Mamlaka za mapato, Bima na Hifadhi ya Jamii.

Kwahiyo lazima tuzingatie kuwa watu wote na taasisi zote hizo zinatutegemea katika kufanikisha mfumo huu wa Anuani za Makazi na Postikodi.  Tafadhali tusiwaangushe.

7.0 HUDUMA YA POSTA MLANGONI

Mwenyekiti na Wajumbe,

Kwa kuzingatia mwelekeo huu, Shirika hili limeanzisha huduma mpya ijulikanayo kama “POSTA MLANGONI”.  Huduma hii tajwa imeanzishwa hapa Dar es Salaam, Dodoma na Arusha.

Ni mwanzo mzuri, lakini ningependa mwongeze jitihada katika jambo hili.  Mwelekeo wetu uwe ni kuzingatia maslahi mapana ambayo ni pamoja na:-

·         Kujenga nchi ya viwanda.

·         Kufikiwa malengo ya Dira ya Taifa ya mwaka 2025 (Vision 2025).

·         Kupunguza umaskini na kurahisisha utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii.

8.0 UTEKELEZAJI WA MIUNDOMBINU MINGINE

Mwenyekiti na Wajumbe,

Pamoja na utekelezaji wa mfumo wa Anuani za Makazi na Postikodi ili kufanikisha dhamira yetu ya kitaifa, kwa bahati nzuri nchi yetu imefikia hatua ya kuridhisha katika kusimika miundombinu mingine muhimu ya kufanikisha dhamira hii.

Miundombinu hii ni pamoja na:-

·         Upanuzi wa Mkongo wa Taifa na Ujenzi wa mikongo ya mijini (Metro fiber network).

·         Ujenzi wa kituo mahiri cha kutunza kumbukumbu (Data – Centre).

·         Uboreshaji wa mtandao wa barabara, viwanja vya ndege na bandari.

·         Usambazaji wa huduma za nishati ya umeme katika maeneo yote ya nchi yetu.

          Nawaagiza Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti, na Wafanyakazi wote wa Shirika hili           changamkieni fursa za miundombinu hii.

9.0 HITIMISHO

Mwenyekiti,

Kabla ya kumaliza hotuba yangu ningependa kusisitiza juu ya maeneo yafuatayo:-

·         Uwajibikaji, uchapakazi na ubadilishwaji wa mtazamo (change of mind sets) ya wafanyakazi wa Shirika hili.  Tuondokane na kuendesha shughuli zetu kwa mazoea (business as usual).  Hii ni pamoja na kuwajengea uwezo katika teknolojia ya kisasa.

·         Kuongeza udhibiti wa usalama katika mtandao wa Shirika.  Tuwe macho na uhalifu wa kimtandao kama usafirishaji wa madawa ya kulevya, utakatishaji wa fedha na uzingatiaji wa jumla wa sheria za nchi na Kimataifa.

·         Kuanzisha huduma ya “One Stop Community Centre”.  Hii iende sambamba na kuimarisha huduma za uwakala kwa kutumia TEHAMA ikiwa ni pamoja na kuwa na “Payment Switch”.

·         Eneo lingine ni kutoa huduma bora zinazowaridhisha wateja (customer satisfaction).  Hii ni pamoja na kuimarisha shughuli zenu za masoko.

·         Kupanua wigo wa biashara, kuongeza mapato, kupata faida na hatimaye kutoa gawiwo kwa mwenye hisa ambaye ni serikali.

Nafahamu baadhi ya mambo haya yako katika mipango yenu ila la muhimu ni ufuatiliaji na  utekelezaji wenu. Kwa upande wa Serikali tunatambua na kuzingatia changamoto za msingi za Shirika hili ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mtaji na mzigo wa kulipa pensheni za wastaafu wa Jumuiya ya zamani ya Afrika Mashariki.

Baada ya kuyasema hayo, sasa natamka kuwa – Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Posta Tanzania, IMEZINDULIWA RASMI.


Ahsanteni kwa kunisikiliza
Post a Comment