JAJI KIONGOZI AWATAKA MAJAJI KUTENDA HAKI

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mheshimiwa Ferdinand Wambali akifungua Mkutano wa Majaji Wafawidhi na Majaji waliosikiliza Kesi za Uchaguzi wa mwaka 2015 unaofanyika jijnini Arusha. 

Baadhi ya Waheshimiwa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Kutathmini usikilizwaji wa kesi za uchaguzi unaofanyika jijini Arusha. 

Baadhi ya Waheshimiwa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Kutathmini usikilizwaji wa kesi za uchaguzi unaofanyika jijini Arusha. 

…………………………………………………………. 

Na Lydia Churi- Mahakama 

Majaji wa Mahakama Kuu nchini wametakiwa kufanya kazi yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo wakati wote kwa kuwa watanzania wanaitegemea Mahakama kuwatendea haki kwa sawa na kwa wakati. 

Akifungua Mkutano wa Majaji Wafawidhi na Majaji waliosikiliza kesi za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 unaotathmini usikilizwaji wa kesi hizo leo jijini Arusha, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mheshimiwa Ferdinand Wambali alisema watanzania wana imani na Mahakama hivyo ni muhimu kwa Majaji hao kutenda haki wakati wote. 

Alisema Majaji hao wamekutana ili waweze kupata nafasi ya kujadili changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa kusikiliza kesi zilizohusu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kubadilishana mawazo namna ya kuzimaliza kwa haraka kesi zihusuzo uchaguzi kwa siku za mbeleni. 

Alisema jumla ya kesi 53 za Ubunge zilizotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zilifunguliwa katika Mahakama Kuu kanda za Dar es salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Moshi, Mtwara na Mwanza. Kanda nyingine ni Shinyanga, Songea, Sumbawanga, na Tanga. 

Jaji Wambali alisema kati ya kesi hizo, kesi 31 zilimalizika katika hatua za awali na kesi 22 ziliendelea. Mpaka sasa kesi 19 zimemalizika. Aliongeza kuwa kesi tatu bado ziko mahakamani. 

Jaji Wambali alisema ni jambo la kujivunia kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuwa kesi zote 196 zilizotokana na uchaguzi wa madiwani zilimalizika mapema katika Mahakama mbalimbali za Hakimu Mkazi nchini. 

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kufanyika kwa uchaguzi Mkuu nchini, zaidi ya asilimia 94 ya kesi za uchaguzi zilizofunguliwa kwenye Mahakama Kuu zimemalizika wakati asilimia 100 ya kesi zote za udiwani zimemalizika. 

Jaji Kiongozi amewapongeza Majaji na Mahakimu wote kwa kumaliza kesi kwa ufanisi na kwa wakati licha ya changamoto mbalimbali wanazozipitia Watumishi hao wa Mahakama wakati wanaposikiliza kesi zainazotokana na uchaguzi. 

Aidha Jaji Kiongozi alishukuru shirika la Umoja wa Mataifa-UNDP kwa kufadhili mafunzo mbalimbali ya Majaji na Mahakaimu yaliyotolewa kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Mkutano wa siku nne wa Majaji Wafawidhi pamoja na Majaji waliosikiliza kesi za uchaguzi ulioanza leo jijini Arusha umefadhiliwa na shirika hilo.

Comments